1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN kupeleka walinda amani zaidi Sudan

17 Novemba 2010

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuenea kwa mzozo wa Sudan na kuitaka serikali ya nchi hiyo kuharakisha mchakato wa matayarisho ya kura ya maoni ya Januari 9 mwakani

https://p.dw.com/p/QAvf
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-MoonPicha: picture-alliance / dpa

Akikihutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichofanyika jana mjini New York, Marekani bwana Ban alisema umoja huo unapanga kupeleka wanajeshi zaidi wa kulinda amani nchini Sudan, huku kura ya maoni ikitarajiwa kufanyika Januari 9 mwakani. Ban Ki Moon, alizungumzia kuhusu kauli za uhasama zinazotolewa hadharani na madai ya kukiukwa mkataba wa kusitisha mapigano, hali inayotishia kuongeza wasiwasi na kuchochea matukio ya kuvuruga usalama yanayoweza kusababisha mzozo mpana zaidi.

Bwana Ban amesema Umoja wa Mataifa unashauriana na Sudan kaskazini na kusini juu ya kupeleka wanajeshi zaidi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kuimarisha usalama wakati wa kura ya maoni na baada ya kufanyika kura hiyo. Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan, UNAMID, kwa sasa kina wanajeshi 10,000.

Hata hivyo Ban amesisitiza kuwa vikosi vya umoja huo nchini humo havitatosha kuzuia kuzuka tena vita, iwapo kutatokea machafuko katika sehemu nyingi. Amesema machafuko yanatarajiwa kutokea katika jimbo la Abyei ambako kuna hofu kura ya maoni huenda isifanyike kama ilivyopangwa.

"Nabakia kuwa na wasiwasi kuhusu kucheleweshwa kwa matayarisho kunakotokana na upungufu wa fedha. Vikwazo vyote vilivyobakia vinatakiwa kuondolewa ili tume inayosimamia kura ya maoni iweze kugharamia shughuli zake, kuteua na kuwapa mafunzo maafisa inayohitaji na kupitisha maamuzi muhimu bila kuchelewa."

Bwana Ban aidha amesema jumuiya ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali na wafadhili, iko tayari kutoa msaada zaidi kwa Sudan. Amesema mashirika ya misaada yameweka mikakati madhubuti kutoa misaada iwapo kutatokea machafuko wakati ya kura ya maoni.

Hillary Clinton
Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Marekani, Hillary ClintonPicha: picture alliance / abaca

Akiuhutubia mkutano wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, kwa upande wake alisema kura ya maoni ya Januari 9 ni muhimu kwa amani ya Sudan.

"Ni muhimu kwa amani na uthabiti, sio tu kwa Sudan, bali pia kwa nchi jirani na Afrika kwa ujumla, kwamba kura ya maoni ya Sudan kusini ifanyike kwa amani na wakati uliopangwa. Na bila kujali matokeo, ridhaa ya raia lazima iheshimiwe na pande zote nchini Sudan na ulimwenguni kote."

Bi Clinton alisema kama Sudan itafanya kura ya maoni kama ilivyopangwa, kuyaheshimu matokeo na kupata ufumbuzi wa hatma ya jimbo la Abyei, basi Marekani itaifuta Sudan kutoka kwa orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi.

Taarifa ya mkutano wa baraza la usalama kuhusu Sudan iliyosomwa na waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza, William Hague, imeelezea wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la machafuko katika jimbo la Darfur na kukwama kwa mazungumzo ya amani kati ya makundi ya waasi na serikali ya Khartoum.

"Baraza la usalama lina wasiwasi kuhusu mashambulio dhidi ya raia yanayofanywa na wapiganaji na linataka ufadhaili wote wa makundi ya wapiganaji ukome. Linayahimiza makundi yote ya waasi kujiunga na mchakato wa amani bila kuchelewa wala masharti, na pande zote zikomeshe mara moja uhasama na kushiriki katika mazungumzo kwa lengo la kutafuta amani ya kudumu Darfur"

NO FLASH William Hague Außenminister Großbritannien
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Uingereza, William HaguePicha: AP

Baraza la usalama limeitaka serikali ya Sudan kushirikiana zaidi na tume ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani Darfur na kuwapa wanajeshi wa kulinda amani wa umoja huo na wafanyakazi wa mashirika ya misaada, uhuru wa kutembea wanakotaka pasipo kuwazuia.

Mwandishi: Josephat Charo

Mhariri: Aboubakar Liongo