1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN kuidhinisha wajumbe wapya wa Libya na Mashariki ya kati

Amina Mjahid
15 Desemba 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewapendekeza wajumbe wapya watakaoongoza majadiliano ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa Libya na Mashariki ya Kati, ambao huenda wakapewa idhini leo.

https://p.dw.com/p/3mkB7
Nickolay Mladenov UN Friedensbeauftragter Mittlerer Osten
Picha: picture-alliance/NurPhoto/M. Fathi

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amempendekeza mjumbe wake wa sasa wa Mashariki ya Kati, Nickolay Mladenov, kuwa mjumbe wake Maalum upande wa Libya akichukua nafasi ya Ghassan Salame aliyejiuzulu mwezi Machi kufuatia msongo wa mawazo.

Guterres pia amemteua mwanadiplomasia wa miaka mingi wa Norway, Tor Wennesland, kuchukua nafasi ya Mladenov ya mpatanishi wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro kati ya Israel na Plaestina.

Iwapo wajumbe hao waliochaguliwa hawatopingwa na mwanachama yoyote kati ya wanachama 15 wanaounda Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ifikapo leo jioni, basi uteuzi huo utaidhinishwa moja kwa moja.

Hatua hiyo itamaliza mizozano ya miezi mingi iliyoanzishwa na Marekani, kushinikiza kugawana majukumu ya Libya ili pawepo na mtu mmoja anayeshughulikia masuala ya kisiasa, na mwengine anayeshughulikia masuala ya upatanishi katika migogoro.

UN-Sicherheitsrat
Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: picture-alliance/Photoshot/Li Muzi

Pande hasimu zakubaliana kusitisha mapigano Libya

Libya iliingia katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikubaliana na mpango huo mwezi Septemba. Muda mfupi baadaye Guterres akampendekeza mwanadiplomasia wa Bulgaria Mladenov kuchukua jukumu la Libya mwezi uliopita na siku ya Ijumaa akamchagua Wennesland, ambaye kwa sasa ni mjumbe wa Norway katika masuala ya kutafuta amani ya Mashariki ya Kati, kuchukua nafasi ya Mladenov, hii ikiwa ni kwa mujibu wa barua zilizoonekana na shirika la habari la Reuters.

Mladenov amekuwa mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Mashariki ya Kati kuanzia mwaka 2015.

Libya ilitumbukia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe baada ya Jumuiya ya kujihami ya NATO kuunga mkono hatua ya kumpindua kiongozi wa muda mrefu wa taifa hilo Muammar Gaddaffi mwaka 2011.

Mwezi Oktoba, pande mbili hasimu katika mgogoro huo, serikali inayotambuliwa kimataifa na serikali ilioko mashariki mwa Libya inayoongozwa na Khalifa Haftar, zilikubaliana kusitisha mapigano. Haftar anaungwa mkono na Umoja wa falme za kiarabu, Misri na Urusi huku serikali iiungwa mkono na Uturuki.

Kwa upande mwengine, katika mgogoro wa Mashariki ya Kati, Wapalestina wanataka kuunda dola lao upande wa Ukingo wa Magharibi, Mashariki mwa Jerusalem na Ukanda wa Gaza, maeneo ambayo Israel iliyateka katika vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka wa 1967.