1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umuhimu wa vyombo vya habari kuripoti Maendeleo 17 endelevu

Sylvia Mwehozi
10 Novemba 2016

Vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kuripoti taarifa zinazohusiana na malengo mapya 17 ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa ambayo yamepangwa utekelezaji wake kukamilika ifikapo mwaka 2030

https://p.dw.com/p/2RyBq

Baada ya kupitishwa na kuridhiwa na mataifa zaidi ya 160, malengo mapya 17 ya Maendeleo Endelevu yanatajwa kugusa kila sekta ikiwemo kuutokomeza umaskini na njaa, usawa wa kijinsia na masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi. Mkurungenzi wa shirika la habari la IPS Falhana Haque Rahman akizungumza na DW amesema maendeleo endelevu yanatoa fursa kwa nchi na dunia kwa ujumla kutokomeza umaskini na kuhakikisha kwamba haki za binadamu zinaheshimiwa, mfano haki ya kupata elimu, afya, maji safi na salama, kazi nzuri, na amani. Mkurugenzi huyo anaeleza zaidi kwamba malengo haya ni mwendelezo wa hatua na mafanikio yaliyokwisha patikana na kwa hivyo vyombo vya habari vina wajibu mkubwa katika mapambano hayo. 

Bi Rahman anasema kwamba "Ni muhimu sana kwasababu mwisho wa siku ni kwa ajili ya watu kufahamu nini kinatakiwa. Ikiwa watu hawana ufahamu nini kinatarajiwa kutoka kwao, kama hakuna ufahamu, hakuna uelewa wa masuala yaliyomo na yapi yanaweza kuwa madhara basi tutashindwa kuyafikia malengo. Na kiungo muhimu cha kuyafikisha haya kwa wananchi, watunga sera ni kupitia vyombo vya habari na vyombo vya habari vina nguvu." 
Maendeleo endelevu yamedhamiria katika miaka 15 ijayo kuleta uwiano wa maendeleo katika nchi moja moja na kwa ujumla ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na umaskini ambayo ndio malengo ya haraka. Kila nchi itapaswa kuwa na mpango mkakati wa namna ya kutekeleza baadhi ya malengo, ikiwa ni vigumu kuyatekeleza yote kwa mpigo. Hata hivyo changamoto ya kifedha ndio inatajwa kuziangusha nchi zinazoendelea, kama anavyoeleza Thalif Deen mshauri mwandamizi na mkuu wa zamani wa ofisi ya IPS katika Umoja wa Mataifa. "Unajua nchi zinazoendelea zinahitaji fedha za ufadhili kwa ajili ya utekelezaji, kwa mfano tuseme kutokomeza umaskini au njaa, kwa hiyo inategemea ni kiasi gani cha fedha wanaweza kukusanya na tayari wanazungumza matilioni ya dola ambayo yanahitajika, ni kati ya tilioni 3 hadi 5 ili kutekeleza kikamilifu malengo endelevu. Na katibu mkuu anasema hili linahitaji ufadhili, kwanza wa mataifa yaliyo tajiri kiviwanda na pili anategemea kutoka kwa sekta binafsi."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: Reuters/M. Segar

Lengo mojawapo ni upatikanaji wa elimu bora kwa wote ambapo kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ya ufuatiliaji wa elimu kidunia mwaka 2016, inaonyesha kuwa kwa mwaka 2014 watu milioni 263 wakiwemo watoto, watu wazima na vijana walikuwa nje ya shule katika kiwango cha elimu ya msingi na ile ya sekondari. Pembezoni nazungumza na Miki Nazowa , kutoka kituo cha kimataifa cha ufundi, stadi na mafunzo UNEVOC kuhusu lengo hili. "Malengo endelevu kuhusu elimu hayalengi tu elimu ya msingi bali yanahusu nyanja zote. Hapa tunazungumzia misingi ya upatikanaji elimu kama haki ya msingi ya binadamu, na mafunzo endelevu kwa hiyo tunaweza sema haya tunaendelea nayo na pia suala la usawa na ushirikishwaji katika elimu ni vipengele muhimu."

Malengo 17 endelevu yalianzishwa baada ya kumalizika malengo nane ya milenia mnamo mwaka jana mabapo baadhi ya nchi hususan za kusini mwa Afrikazilishuhudiwa zikipiga hatua katika baadhi ya malengo ikiwemo suala la kuwaandikisha watoto shule waliofikia umri wa kuanza shule. 
Mwandishi: Sylvia Mwehozi
Mhariri: Iddi Ssessanga