1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya yaiwekea vikazo vikali zaidi Iran

17 Juni 2010

Urusi yasema vimeegemea upande mmoja

https://p.dw.com/p/Ntnj
Rais wa Iran Mahmoud Ahmeidnejad akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya kigeni wa Urusi Sergey Ryabkov.Nchi hizo mbili zimekuwa na uhusiano wa karibu kibiashara.Picha: AP

Wakuu wa nchi na serikali kutoka Umoja wa ulaya,leo wamekubaliana kupitisha vikwazo vipya kwa Iran,katika sekta ya biashara ili kuishinikiza nchi hiyo kuachana na mpango wake wa kinyuklia.

Vikwazo hivyo vinajumuisha sekta ya mabenki na makampuni ya Iran yanayojishughulisha na usafiri wa anga na mizigo,vikwazo ambavyo vimepingwa vikali na Urusi ambayo imeelezea kuwa ni vya upande mmoja,ikisema imesikitishwa.

Urusi ambayo imekuwa na uhusiano wa karibu na Iran kibiashara,mwezi mmoja uliopita ilikubaliana na msimamo wa baraza la usalama la umoja wa mataifa juu ya kuwekewa vikwazo Iran,lakini imeelezea kusikitishwa na uamuzi wa baraza la umoja wa ulaya,kuweka vikwazo vikali zaidi katika sekta ya biashara.

Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Ryabkov ameonya kuwa vikwazo hivyo vipya dhidi ya Iran,ni dalili kwamba umoja huo wa Ulaya umejiweka juu ya baraza la usalama la umoja wa mataifa vilivyotolewa juni 10 mwaka huu,hali itakayohatarisha uhusiano wao,katika kulitanzua suala hilo.

Urusi inatajwa kuwa itaweza kuathirika zaidi kibiashara kufuatia uamuzi huo wa umoja wa ulaya,lakini pia Ujerumani ambayo imewekeza zaidi nchini Iran katika sekta ya mafuta na gesi nayo imetajwa kukumbwa na athari hiyo.

Nchi hiyo imeeleza kuwa licha ya jitihada zake za kuzishawishi Marekani na Umoja huo kutoweka vikwazo vikali zaidi ya vile vilivyotolewa na baraza la usalama,lakini amesema kuwa wazo lao limepuuzwa.

Imearifiwa baada ya kikao cha wakuu wa serikali za umoja wa Ulaya kuwa vikwazo hivyo vitaanza kufanya kazi katika kipindi cha wiki chache zijazo,ambapo vikwazo hivyo vitazuia uwekezaji pamoja na msaada wa kitaalamu kutoka jumuiya hiyo.

Iran licha ya kuwa na hazina kubwa ya mafuta,inatajwa kuwa ni nchi ya tano duniani kwa usafirishaji wa mafuta yasiyosafishwa,kutokana na kukosa teknolojia hiyo ndani ya nchi,imeelezwa kuwa vikwazo hivyo vitaiathiri kiuchumi.

Hatua hiyo kuwekewa vikwazo hivyo inakwenda mbali zaidi na kile wanadiplomasia walichokitarajia na huenda ikaipa shinikizo kubwa Iran panapohusika na pato lake la fedha linalotokana na mafuta , ikiwa ni mtoaji wa tano mkubwa wa mafuta duniani.

Wakati taarifa za kuongezewa vikwazo Iran na umoja wa ulaya zikitolewa,Iran imesaini mkataba wa kuagiza gesi kutoka Turkmenistan kwa kiasi ya asilimia 40 na kufikia kubik mita bilioni 14.

Kwa mujibu wa naibu waziri wa mafuta wa Iran, Javad Ouji, kulingana na mkataba huo mpya inakadiriwa uagizaji gesi kwa siku utafikia kubik mita milioni 40 ifikapo msimu wa baridi mwaka huu.

Bomba jipya la kusafirishia gesi kutoka Turkmenistan hadi Iran lilifunguliwa na Rais Ahmedinejad mwezi Januari.

Mwandishi; Ramadhan Tuwa/ AFPE/RTRE

Mhariri; Abdul-Rahman