1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya watoa euro milioni 2 Philippines

29 Septemba 2009

Ni katika kuwasaidia waathirika wa mafuriko

https://p.dw.com/p/Jtg8
Moja ya familia zlizoathirika na mafuriko katika eneo la Pasig, mashariki mwa Manila nchini Philippines.Picha: AP

Umoja wa Ulaya umesema leo kuwa utatoa kiasi cha uero milioni 2 kama msaada wa dharura kwa waathirika wa mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa na kimbunga cha Ketsana, ambacho kumeua angalau watu 240 na kusababisha maelfu kwa maelfu kupoteza makazi yao nchini Philippines.

Fedha hizo ambazo zitatolewa na Tume ya Ulaya mjini Brussels, zitasaidia kukidhi mahitaji muhimu ya waathirika hao, kama vile chakula, maji safi ya kunywa, afya na makazi ya muda.

Mahitaji hayo yameoorodheshwa kuwa ni ya muhimu zaidi kwa sasa na kundi la maafisa wawili wa Idara ya Misaada ya kibinadamu ya Tume hiyo, ambao kwa sasa wapo katika mji mkuu wa Philippines, Manila.

Afisa wa idara hiyo Karel De Gucht, amesema msaada huo wa haraka unaotolewa, utazingatia katika maeneo yaliyo katika hali mbaya zaidi.

Miradi inayofadhiliwa na Tume ya Umoja wa Ulaya, hutekelezwa na mashirika yasiyo ya kiserikali, mashirika maalumu ya Umoja wa Mataifa pamoja Msalaba Mwekundu.

Wakati hayo yakijiri, leo kumeripotiwa kuwa kimbunga hicho kimelikumba eneo la pwani ya kati ya Vietnam, na kusababisha vifo vya watu 22 na wengine 170,000 kuyakimbia makazi yao.

Vifo vya watu hao nchini Vietnam, ni ongezeko la watu 246 waliopoteza maisha yao kutokana na mafuriko hayo nchini Philippines, ambayo yameuharibu kabisa mji mkuu wa nchi hiyo Manila.

Watu tisa kati ya waliokufa waliporomoshwa na ardhi katika jimbo la Kon Tum lililoko milimani, na nyumba zao kuharibiwa vibaya na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali.

Afisa mmoja wa wilaya ya Phu Vang, amesema kuwa wana wasiwasi hatari inayosababishwa na mafuriko hayo, inaweza ikawa mbaya zaidi, kwa sababu mvua zinazoendelea kunyesha zinaongeza kiwango cha maji katika mito, lakini zaidi zinaongeza kiwango cha maji ya bahari na hivyo kutishia maisha ya wakazi wa maeneo ya pwani.

Mwandishi habari wa Shirika la Habari la AFP amesema mafuriko hayo yameuharibu kabisa mji mkuu wa zamani wa jimbo hilo, pamoja na ofisi ya Urithi wa Dunia ya UNESCO, ambapo waathirika walikuwa wanatumia vipande vidogo vya mbao na mabati kuelea kwenye maji.

Miti iliyoanguka barabarani imeifunga kabisa mitaa pamoja na mito kufurika, wakati ambapo kasi ya upepo nayo imeongezeka maradufu, huku maji yakiendelea kutiririka yakifuata njia ya reli.

Rais wa serikali za mitaa Nguyen Ngoc Thien, amesema karibu abiria 1,000 wamekwama katika kituo cha treni cha Hue katika jimbo la Thua Thien-Hue.

Eneo hilo pia ndipo ulipo mtambo wa kuchakatia mafuta uliofunguliwa mwezi Februari mwaka huu, ambao hata hivyo haukuharibiwa na kimbunga hicho.

Televisheni ya nchi hiyo imesema Mamlaka zimepoteza mawasiliano kabisa na kisiwa cha Ly Son, kilichopo katika bahari ya Kusini China.

Mwandishi: Lazaro Matalange/AFP

Mhariri: Abdul-Rahman