Umoja wa Ulaya wataka makubaliano ya kibiashara na mataifa ya Ghuba | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 08.05.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Umoja wa Ulaya wataka makubaliano ya kibiashara na mataifa ya Ghuba

Mkutano wa 17 baina ya mawaziri wa nchi za Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wa baraza la ushirikiano wa Guba ulifanyika jana mjini Riyadh Saudi Arabia. Mada mbiu ya mkutano huo ilihusu biashara huru kati ya kanda hizo mbili za kibiashara.

Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia

Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia

Tayari wakati wa ziara ya mwisho ya kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye pia ni rais wa Umoja wa Ulaya, katika eneo lililonawiri kiuchumi la Ghuba, ari ya kisiasa katika Umoja wa Ulaya na mataifa ya Ghuba ilidhihirika wazi. Umoja wa Ulaya na mataifa ya Ghuba yanataka kufanikisha kusainiwa kwa mkataba wa biashara huru.

Mazungumzo baina ya pande hizo mbili yalivunjika wakati wa msimu wa kiangazi mnamo mwaka jana kwa sababu Umoja wa Ulaya uliyapendekezea mataifa ya Ghuba kuyafungua kwa kiwango kidogo masoko yake ya fedha na kutaka kiwango kikubwa cha uwekezaji wa Ulaya katika nchi hizo. Lakini baada ya kumaliza tofauti zilizokuwepo sasa inwezekana mkataba wa kwanza wa kibiashara kuanza kutekelezwa ifikapo mwezi Januari mwaka ujao.

Katika mkutano wa mjini Riyadh upande mmoja waliketi wajumbe wa Umoja wa Ulaya na upande wa pili wajumbe wa mataifa wanachama wa baraza la Ghuba, yakiwemo Kuwait, Bahrain, Saudi Arabia, Katar, Umoja wa falme za kiarabu na Oman. Baraza hilo lilianzishwa mnamo mwaka wa 1981 kufuatia ari ya Iran kutaka kuendeleza sera yake ya mapinduzi.

Lengo kubwa la muungano huo ni kuboresha ushirikiano wa pamoja katika sera za nje na za usalama vilevile ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama. Tangu kuanza kwa sarafu ya euro barani Ulaya nchi za baraza la Ghuba zinataka kufikia muungano wa kisarafu na kiuchumi. Ikiwa jambo hilo litaweza kufikiwa hivi karibuni, soko la Ulaya huenda likapanuka zaidi.

Ukweli ni kwamba uhusiano baina ya Umoja wa Ulaya na baraza la Ghuba umekita katika uwezo wa kujitegemea kiuchumi na katika mahitaji ya nishati. Umoja wa Ulaya unasimamia usambazaji wa nishati katika mataifa ya baraza la Ghuba na ni soko muhimu la sehemu kubwa ya bidhaa zake. Hivyo Umoja wa Ulaya una jukumu muhimu katika mataifa hayo.

Mwaka wa 2004 mauzo ya bidhaa za Umoja wa Ulaya katika mataifa ya Ghuba yalifikia euro bilioni 40. Bidhaa zinazouzwa katika nchi za Umoja wa Ulaya kutoka eneo la Ghuba zilifikia kima cha euro 25. Kwa hiyo Umoja wa Ulaya ni muwekezaji mkubwa katika nchi wanachama wa baraza la Ghuba.

Sasa mazungumzo ya kujaribu kufikia mkataba wa biashara huru ni sababu kubwa ya kuongezeka uhusiano wa kisiasa kati ya Umoja wa Ulaya na mataifa ya baraza la Ghuba. Mbali na uhusiano wa kichumi na na kibiashara Umoja wa Ulaya unataka kujenga ushirikiano katika usalama wa nishati, utamaduni, elimu na ulinzi wa mazingira. Lakini la muhimu zaidi ya yote ni uhusiano wa kisiasa na kiusalama hususan katika swala la kupambana na ugaidi.

Mkataba wa kibiashara kwa kipindi kirefu unaanzisha hatua muhimu katika safari ndefu kufikia ushirikiano muhimu baina ya Umoja wa Ulaya na mataifa wanachama wa baraza la Ghuba.

Kwa mujibu wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya kusainiwa kwa mkataba wa kibiashara baina ya umoja huo na mataifa ya Ghuba huenda kukaongeza marudufu kiwango cha mauzo ya bidhaa katika mataifa ya pande hizo mbili katika kipindi kifupi. Hata hivyo isieleweke vibaya kwamba Umoja wa Ulaya hauna mkakati maalmu katika eneo hili muhimu la Ghuba.

 • Tarehe 08.05.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB4F
 • Tarehe 08.05.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB4F

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com