Umoja wa Ulaya watafakari msaada kwa Mali | Matukio ya Afrika | DW | 28.09.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Umoja wa Ulaya watafakari msaada kwa Mali

Umoja wa Ulaya unatafakari namna ya kuisaidia Mali kupambana na wanamgambo wa kiislamu wanaodhibiti sehemu ya Mali kaskazini, baada ya kupokea maombi ya msaada kutoka kwa serikali ya nchi hiyo.

Wanamgambo wa Kiislamu wakifanya doria katika mji wa Gao.

Wanamgambo wa Kiislamu wakifanya doria katika mji wa Gao.

Taarifa iliyotolewa na Cyprus, ambayo inashikilia urais wa Umoja wa Ulaya, imesema kuwa mawaziri wa ulinzi wa umoja huo waliokutana katika mji mkuu wa nchi hiyo, Nicosia, wamewataka maafisa wa umoja huo kubainisha njia ambazo umoja huo unaweza kupitia kuunga mkono juhudi za kimataifa kuisadia Mali. Mali ilitumbukia katika vurugu mwezi Machi mwaka huu kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa rais Amadou Touman Toure na kuacha pengo la uongozi lililowapa mwanya waasi wa Tuareg kuteka karibu theluthi mbili ya nchi hiyo.

Ramani hii inaonyesha mataifa yaliyokuwa chini ya utawala wa ufaransa na eneo linalodhibitiwa na waasi (misitari ya njano) nchini Mali .

Ramani hii inaonyesha mataifa yaliyokuwa chini ya utawala wa ufaransa na eneo linalodhibitiwa na waasi (misitari ya njano) nchini Mali .

Tangu wakati huo makundi ya wanamgambo wa kiislamu yametumia uasi huo kulazimisha utawala wa sharia na kuzusha hofu kwamba yanaweza kuivuruga kanda hiyo zaidi. Serikali dhaifu ya mpito, ambayo inashikilia mji mkuu wa Bamako, imeliomba baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuruhusu kutumika kwa nguvu za kijeshi kaskazini mwa nchi hiyo. Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, imesema iko tayari kupeleka vikosi.

ECOWAS, Mali watuma maombi tofauti

Naibu katibu mkuu wa idara ya kutoa huduma za nje ya Umoja wa Ulaya, Maciej Popowski, aliwambia wandishi wa habari baada ya mkutano wa mawaziri wa ulinzi, kuwa umoja huo umepokea maombi kutoka jumuiya ya ECOWAS kusaidia operesheni yake nchini Mali na pia umepokea maombi mengine tofauti kutoka serikali ya mpito ya mali kuisaidia kulisuka upya jeshi lake. Popowski alisema kuwa umoja huo unaendela kuchambua maombi hayo, na kuongeza kuwa mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya watayajadili maombi hayo katika mkutano wao wa Luxembourg Oktoba 15. Alisema Umoja wa Ulaya uko tayari kuchukua jukumu la kuratibu juhudi za kimataifa katika kutatua mgogoro huo.

Wapiganaji wa kundi la Vuguvugu la Umoja na Jihadi Afrika Magharibi (MUJAO) wakitembea katika mitaa ya mji wa Gao, kaskazini mwa Mali.

Wapiganaji wa kundi la Vuguvugu la Umoja na Jihadi Afrika Magharibi (MUJAO) wakitembea katika mitaa ya mji wa Gao, kaskazini mwa Mali.

Afisa moja wa Umoja wa Ulaya, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema Mali iliuomba umoja huo kuisaidi kutoa mafunzo kwa wanajeshi wake na kuipatia vifaa vya kutegua mabomu ya ardhini na pia msaada wa katika usafiri. Umoja wa Ulaya hauzungumzii kupeleka wanajeshi kuwa sehemu ya jeshi la kimataifa, lakini maafisa wanasema kama umoja huo utakubali kuwapatia mafunzo wanajeshi wa Mali. Hili litahitaji wakufunzi wa kijeshi. Hakuna waziri katika mkutano wa Nicosia aliyepinga suala la kuisaidia Mali, lakini kulikuwepo hisia tofauti, alisema afisa huyo wa Umoja wa Ulaya.

Umoja wa Ulaya unasubiri matokeo ya mjadala wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kabla ya kuanza kufanya mipango mahsusi ya kuisaidia Mali. Wanachama wa Umoja wa Mataifa walionekana kuwa na mgawanyiko mkubwa juu ya mgogoro wa Mali siku ya Jumatano, ambapo Ufaransa na baadhi ya majirani wa Mali waliunga hatua za kijeshi, wakati Marekani ilisema Mali lazima kwanza iwe na serikali iliochaguliwa na wananchi.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre
Mhariri: Othman Miraji