Umoja wa Ulaya wapata viongozi wapya | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.09.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Ulaya wapata viongozi wapya

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamemteuwa Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk kuwa rais mpya wa umoja huo na waziri wa mambo ya nje wa Italia Federica Mogherini kuwa mkuu wa sera za kigeni.

Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk na waziri wa mambo ya nje wa Italia Federica Mogherini baada ya kuchaguliwa kushika nyadhifa muhimu za Umoja wa Ulaya Brussels. (30.08.2014)

Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk na waziri wa mambo ya nje wa Italia Federica Mogherini baada ya kuchaguliwa kushika nyadhifa muhimu za Umoja wa Ulaya Brussels. (30.08.2014)

Tusk ambaye anazungumza Kingereza cha kusita sita na hazungumzi Kifaransa ni mwananchi wa kwanza wa Ulaya mashariki kushika wadhifa mkubwa kama huo katika umoja huo na anajulikana kwa ukosoaji wake mkali dhidi ya Urusi hususan kuhusiana na mzozo wa Ukraine.

Rais wa sasa wa Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy amesema muda mfupi baada ya kutolewa tangazo hilo Jumamosi (30.08.2014) usiku kwamba kazi imeanza na timu mpya ya uongozi wa Umoja wa Ulaya imekamilika.

Amesema viongozi hao wapya watakabiliwa na changamoto kuu tatu : kukwama kwa uchumi wa Ulaya,mzozo wa Ukraine ambao ameuita kuwa "tishio baya kabisa kwa usalama wa bara la Ulaya kuwahi kushuhudiwa tokea Vita Baridi" na nafasi ya Uingereza katika Umoja wa Ulaya.

Umuhimu wa umoja Ulaya

Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk (kushoto)na waziri wa mambo ya nje wa Italia Federica Mogherini (kulia) wakipongezwa na Rais wa Umoja wa Ulaya anayemaliza muda wake Herman Van Rompuy (katikati) Brussels (30.08.2014)

Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk (kushoto)na waziri wa mambo ya nje wa Italia Federica Mogherini (kulia) wakipongezwa na Rais wa Umoja wa Ulaya anayemaliza muda wake Herman Van Rompuy (katikati) Brussels (30.08.2014)

Tusk mwanasiasa wa sera za mrengo wa kati kulia akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari uliohudhuriwa pia na Van Rompuy na Mogherini amesema kwamba ameingia Brussels kutoka nchi yenye imani kubwa na umuhimu wa Ulaya.

Pia amesisitiza kwamba hakuna mtu mwenye busara atakayewaza kuwepo kwa Umoja wa Ulaya bila ya Uingereza na ameahidi kufanya kila linalowezekana kutimiza madai ya Uingereza ya kutaka mageuzi katika umoja huo.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amesema amefurahishwa na uteuzi wa Tusk na matamshi yake hayo.

Tusk ataanza kuutumikia wadhifa huop hapo tarehe Mosi mwezi wa Disemba wakati Mogherini iwapo ataidhinishwa na Bunge la Ulaya ataanza kazi yake hiyo mpya hapo tarehe Mosi Novemba.

Aungwa mkono na Merkel

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya Brussels.(30.08.2014)

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya Brussels.(30.08.2014)

Akiungwa mkono kwa nguvu na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Tusk mwenye umri wa miaka 57 ni mtu mwenye kupendelea masoko huria barani Ulaya na anatokea katika vuguvugu la chama cha wafanyakazi nchini Poland cha Solidarity kilichokuwa kikipinga muungano wa Kisovieti na amekuwa katika wadhifa wa waziri mkuu tokea mwaka 2007.

Merkel amesema Tusk anakabiliwa na changamoto kubwa na amempongeza kwa kuwa mtu mwenye kufaa kwa wadhifa huo,mwenye kujitolea na mtu mwenye shauku na umoja wa Ulaya ikiwa ni miaka 25 baada ya kuanguka kwa Ukuta wa Berlin na kumalizika kwa Vita Baridi.

Pia atakuwa anaongoza mikutano ya viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya zenye kutumia sarafu ya euro licha ya kwamba kwa miaka mingi amekuwa akihoji busara ya kuzipa mikopo nchi za kanda ya sarafu ya euro zisifilisike na madeni wakati akiwa waziri mkuu na Poland kutokuwa mwanchama wa sarafu hiyo ya pamoja.

Kunowa Kingereza

Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya Brussels.(30.08.2014)

Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya Brussels.(30.08.2014)

Tusk amekanusha kwamba uwezo wake mdogo wa kumudu lugha za kigeni utamkwamisha katika shughuli zake akiwa kama rais wa Umoja wa Ulaya wadhifa ambao unahitaji umahiri kufanikisha muafaka kutokana na kuwepo kwa misimamo inayopingana na kuwaandaa viongozi wa Ulaya kwa mikutano ya kilele ambayo mara nyingi huwa migumu.

Akijibu suali la mwandishi mmoja wa habari na kuonyesha kuwa anaimudu lugha hiyo amesema " Usiwe na wasi wasi.Nitakinowa Kingereza changu na kuwa tayari kwa asilimia 100 hapo Disemba Mosi."

Rais wa Poland Bronislaw Komorowski amesema uteuzi huo wa rais mpya wa Umoja wa Ulaya ni utambuzi wa mafanikio ya Poland na nafasi yake barani Ulaya.

Nguvu mpya

Mogherini waziri wa mambo ya nje wa Italia mwenye umri wa miaka 41 kwa muda mrefu alikuwa amekuwa matumaini ya kuchukuwa nafasi ya Catherine Ashton akiwa kama mkuu wa sera za kigeni za Umoja wa Ulaya ambapo amekuwa akipongezwa na wafuasi wake kuwa ni mtu mpya na kijana kwa Ulaya.

Amekaririwa akisema " Nataraji kujiunga na nguvu mpya ya kizazi kipya cha Ulaya ambapo kipo sio tu miongoni mwa raia wa Umoja wa Ulaya bali pia katika uongozi wa kisiasa wa Umoja wa Ulaya."

Federica Mogherini mkuu mpya wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya.

Federica Mogherini mkuu mpya wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya.

Uteuzi wa Mogherini awali ulikabiliwa na upinzani mkali kutoka nchi za mashariki mwa Ulaya na kutoka kwa maafisa wa Uingereza kwa kumshutumu kwamba hana uzoefu na msimamo wake kwa Urusi ni dhaifu mno.

Huko nyuma aliwekwa kando katika Mkutano wa Kilele wa kwanza wa Umoja wa Ulaya uliofanyika mwezi wa Julai lakini wiki sita baadae baada ya Italia kuunga mkono kwa ushupavu vikwazo zaidi dhidi ya Urusi Mogherini anayezungumza Kingereza na Kifaransa kwa ufasaha nafasi yake ya kuwania wadhifa huo ilikuja kuimarika.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Italia ambaye nchi yake inaandaa mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya hapo mwezi wa Oktoba kujadili njia za kukuza uchumi amesema suala la kupambana na ukosefu wa ajira linapaswa "kuwa kipau mbele cha kwanza kwa uongozi mpya wa Umoja wa Ulaya."

Taarifa ya umoja huo imesema mkutano huo wa kilele wa kukuza uchumi uliopangwa kufanyika Oktoba saba utalenga suala la ajira hususan ajira ya vijana na uwekezaji.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa

Mhariri :Mtullya Abdu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com