1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wakutana wakiwa si wamoja

Mohammed Khelef16 Septemba 2016

Mkutano wa kilele wa mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya unafanyika mjini Bratislava, Slovakia, bila kuijumuisha Uingereza, ambayo iliamua kujiondoa kwenye muungano huo unaokabiliwa sasa na changamoto ya wakimbizi.

https://p.dw.com/p/1K3m1
Kutoka kushoto: Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Kansela Christian Kern wa Austria wakiwa kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya.
Kutoka kushoto: Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Kansela Christian Kern wa Austria wakiwa kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya.Picha: Reuters/L. Foeger

Licha ya kupiga picha ya pamoja, kupeana mikono na kupanda mashua ya kifahari wakila chakula chao cha mchana kwenye Mto Danube, ukweli haukuweza kujificha kuwa viongozi wakuu wa mataifa 27 wanakabiliwa na wakati mgumu sana kwenye kuudumisha Umoja wao. Katika yote, suala la mgawanyo wa wakimbizi wanaoingia kwenye Umoja wa Ulaya linaonekana kuupasua muungano wao vipande vipande, huku wakiwa hata hawajaafikiana juu ya namna ya Uingereza kujiondoa.

Awali akizungumza na waandishi wa habari nje ya mkutano huo asubuhi ya leo (16 Septemba), Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, taifa ambalo linabeba dhamana kubwa kwenye Umoja wa Ulaya, amekiri kwamba mkutano unafanyika katika kipindi kigumu sana.

"Suala sio kutarajia suluhisho kwa matatizo yote ya Ulaya kwenye mkutano mmoja. Ingawa tupo kwenye hali ngumu sana, mkutano huu unahusiana na kuonesha kwa vitendo kwamba tunaweza kuwa bora zaidi kwenye maeneo ya usalama wa ndani na nje, vita dhidi ya ugaidi, ushirikiano wa kiulinzi." Alisema Kansela Merkel.

Schulz, Orban 'waumana'

Mchana wa leo, tafauti nyengine ilizuka kati ya Hungary, ambayo Waziri Mkuu wake, Viktor Orban, ana msimamo mkali dhidi ya sera ya wakimbizi inayopiganiwa na Ujerumani, na Rais wa Bunge la Ulaya, Martin Schulz.

Hungary imesema itaitisha kura ya maoni kuamua juu ya mgawanyo wa wakimbizi, hatua ambayo Schulz anasema licha ya kuwa haki ya Hungary, bado haibadilishi uhalisia wa matatizo yanayoikabili Ulaya kwa sasa.

"Tatizo la wakimbizi halitapotea kwa kura ya maoni au kuuhamishia Umoja wa Ulaya. Lipo, wakimbizi wanakuja, wanakimbia watokako, nasi lazima tukabiliane na changamoto hii kwa mapendekezo yote ya kulitatua yanakaribishwa."

Kauli ya Schulz ilichukuliwa na Orban kama ni matusi kwa mamlaka ya Hungary, na mbele ya waandishi wa habari kandoni mwa mkutano huo wa kilele, alimtaka Schulz kuwapa heshima wanayostahiki watu wa Hungary.

Viongozi wa mataifa wanachama 27 ya Umoja wa Ulaya katika picha ya pamoja mjini Bratislava, Slovakia.
Viongozi wa mataifa wanachama 27 ya Umoja wa Ulaya katika picha ya pamoja mjini Bratislava, Slovakia.Picha: Reuters/L. Foeger

Waziri Mkuu huyo wa Hungary alisema mawaziri wakuu wa Umoja wa Ulaya walikuwa wamepigia kura mgawanyo wa wakimbizi kwa hiyari, lakini bunge la Ulaya na Kamisheni ya Umoja huo yakaigeuza hiyo kuwa mgawanyo wa lazima.

"Nimemuomba kwa msisitizo mkubwa Rais wa Bunge la Ulaya awaheshimu watu wa Hungary na huko mbeleni ajiepushe na kutumia mbinu za utungaji sheria kuyahujumu maamuzi ya taifa huru na matakwa ya mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya."

La Uingereza 'lawekwa kiporo'

Awali ilitarajiwa suala la kujiondoa kwa Uingereza kwenye Umoja huo lingelikuwa na nafasi muhimu kwenye ajenda, lakini baadaye imefahamika kuwa hakutakuwa na mazungumzo rasmi kuhusu hilo, kwani bado linangojea mchakato wa miaka miwili wa Uingereza yenyewe kusukuma mbele hatua za kujiondoa rasmi.

Hii ni mara ya kwanza kwa Umoja wa Ulaya kufanya mkutano wake wa kilele bila ya ushiriki wa Uingereza, na awali Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk, alisema kwamba licha ya changamoto zilizopo, viongozi wa Umoja huo watakuwa na uthubutu wa kuangaliana machoni, kuambiana ukweli wazi wazi na kusonga mbele.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP, Reuters
Mhariri: Saumu Yussuf