Umoja wa Ulaya wakubaliana kuunda muungano wa Mediterenia | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 14.03.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Umoja wa Ulaya wakubaliana kuunda muungano wa Mediterenia

Makubaliano hayo yanaidhinishwa katika kikao cha leo mjini Brussels Ubelgiji

Vionggzi wa serikali za Umoja wa Ulaya katika mkutano wa mjini Brussels Ubelgiji

Vionggzi wa serikali za Umoja wa Ulaya katika mkutano wa mjini Brussels Ubelgiji

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa hii leo kuidhinishas rasmi pendekezo la Ufaransa la kuundwa kwa muungano wa nchi zinazopakana na bahari ya Mediterenia kuboresha uhusiano na majirani zake wa kusini. Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy anasema ameshinda uungwaji mono wa pendekezo lake.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kuidhinisha rasmi pendekezo la Ufaransa kutaka kuundwe muungano wa nchi zinazopakana na bahari ya Mediterenia ili kuboresha uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na nchi jirani za kusini.

Lakini mpango huo uliopendekezwa na rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa na kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwenye mkutano wa kilele wa wanachama 27 wa Umoja w Uklaya unafana kidogo na ule uliopendekezwa kwanza na Ufaransa.

Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya, Janez Jansa amesema baraza hilo limeidhinisha kanuni za kuundwa muungano wa nchi zinazopakana na bahari ya Mediterenia ambao utazijumulisha nchi wanachama wa umoja wa Ulaya.

"Leo tumekubaliana kwamba ni lazima mkataba uliosainiwa mjini Barcelona nchini Uhispania utathiminiwe. Lakini katika baraza la Ulaya bado hatujakubaliana vipi hasa jambo hilo linavyotakiwa kufanywa.´"

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana kwa siku ya pili mjini Brussels Ubelgiji hii leo. Katika kikao cha leo wanatarajiwa kuidhinisha makubaliano ya kanuni za kuundwa kwa muungano wa nchi za Mediterenia. Wataialika halmashauri ya Umoja wa Ulaya kupendekeza taratibu za kuuzindua muungano huo mpya kwenye mkutano uliopangwa kufanyika mjini Paris Ufaransa mnamo tarehe 13 mwezi Julai mwaka huu.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye amekuwa katika mvutano na Ufaransa kwa miezi kadhaa, ambao uliilazimisha Ufaransa kuondoa vipengele vya pendekezo hilo vilivyozusha utata, ameunga mkono makubaliano yaliyofikiwa mjini Brussels.

´Ndiyo maana ni sawa kwa rais wa Ufaransa kusema tunauweka mzozo huo katika ngazi mpya. Lakini hatuvibadili vipengele vya mkataba huo bali tunatazama tu na kufuatilia kwa karibu hali ya kisiasa katika nchi wanachama kuhakikisha fedha zinatumika hasa kutimiza malengo kulingana na ilivyokuwa imepangwa.´

Wazo la rais mmoja halitafaulu

Wazo la kuwa na muungano wa nchi zinazopakana na bahari ya Mediterenia ukijumulisha mashirika tisa mapya na benki moja, limebadilika na kuwa ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na nchi za Mediterenia utakaokuwa na rais mmoja, wazo ambalo pia huenda likafutiliwa mbali.

Kansela Merkel amesema mpango wa kwanza ungeugawa Umoja wa Ulaya na kusababisha fedha za pamoja zitumiwe kwa manufaa ya wanachama wachache na koloni zao. Lakini rais Sarkozy amesema hakuwa na wazo la kuziacha nje nchi za umoja huo na hakuutazama muungano wa nchi zinazopakana na bahari ya Mediterenia kuwa mpinzani wa umoja huo.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Uhispania anayehusika na maswala ya Umoja wa Ulaya, Alberto Navarro,amesema wazo la kuwa na urais wa kuzunguka katika muungano wa nchi za bahari ya Mediterenia halitafanya kazi kwa kuwa nchi za kiarabu zitakwepa kwenda nchini Israel. Mratibu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana, pia ameeleza wasiwasi huo akisema ipo haja ya kufanya juhudi kuboresha uhusiano kati ya kanda hizo mbili.

"Nafikiri chochote tunachoweza kukifanya kuwa na uhusiano mzuri zaidi kati ya Umoja wa Ulaya na nchi zinazopakana na bahari ya mediterenia sharti tukifanye. Kilicho wazi hivi sasa ni kwamba wanachama wote wa Umoja wa Ulaya watakuwa na jukumu lile lile katika ngazi sawa. Hilo nadhani ndilo wazo jipya lililowasilishwa."

Wanadiplomasia wa Ufaransa wana matumaini mkutano wa mjini Paris utazindua mikataba kadhaa kama vile kuisafisha bahari ya Mediterenia iliyochafuliwa na juhudi za pamoja za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kupambana na mioto inayoharibu misitu.

 • Tarehe 14.03.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DONP
 • Tarehe 14.03.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DONP
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com