Umoja wa Ulaya wakubaliana juu ya Bajeti | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.02.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Ulaya wakubaliana juu ya Bajeti

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kupunguza bajeti ya umoja huo ya mwaka 2014-2020 hadi kufikia Euro bilioni 960 ikiwa ni mara ya kwanza kupunguzwa katika kipindi cha miongo sita.

Baadhi ya viongozi wa Umoja wa Ulaya

Baadhi ya viongozi wa Umoja wa Ulaya

Viongozi hao wamefikia makubaliano hayo leo asubuhi katika mkutano wao mjini Brussels, Ubelgiji, baada ya karibu saa 18, huku masuala yaliyopewa kipaumbele yakiwa ni pamoja na ruzuku ya kilimo, utafiti wa sayansi na misaada. Baadhi ya wanadiplomasia wakisema hatua hiyo imefikiwa kutokana na shinikizo la Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron.

Kiongozi huyo wa Uingereza alikuwa anataka kila nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya kuchangia katika hatua za kubana matumizi huku akiungwa mkono na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron

Cameron ambaye mwezi uliopita alitishia kujitenga na umoja huo kwa kusema ataanda kura ya maoni, aliwasilisha maoni yake mezani mara moja, akionya kuhusu kufikiwa kwa makubaliano. Cameron alisema, ''Tulipokuwa hapa mwezi Novemba mwaka uliopita matumizi ya bajeti yaliyopendekezwa yalikuwa makubwa sana na hivyo yanapaswa kupunguzwa na yasipoponguzwa, hapatakuwa na makubaliano.''

Ufaransa nchi za za Kusini mwa Ulaya zataka kupunguza ukosefu wa ajira

Ufaransa na Italia kwa upande wake zenyewe zilikuwa zikitaka fedha kwa ajili ya kusaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira barani Ulaya katika mazungumzo hayo yanayotarajiwa kukamilishwa baadaye hii leo. Idadi ya watu wasio na ajira barani Ulaya ni zaidi ya watu milioni 26, hiyo ikiwa ni karibu watu watatu kati ya watano wenye chini ya umri wa miaka 25 nchini Uhispania na Ugiriki.

Aidha, viongozi hao walipunguza kiasi cha Euro bilioni 12 kutoka katika mapendekezo ya matumizi ya bajeti yaliyofikiwa mwezi Novemba mwaka uliopita. Awali, Halmashauri Kuu ya Ulaya, chombo kikuu cha umoja huo, kilitaka asilimia 5.0 kuongezwa katika michango ya mataifa wanachama hadi Euro trilioni 1.04 kwa bajeti hiyo ya mwaka 2014-2020, hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia moja ya pato la ndani la Umoja huo.

Rais wa Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy

Rais wa Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy

Hata hivyo, Rais wa Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy, alipunguza fedha hizo hadi Euro bilioni 973 katika mkutano ulioshindwa kufikia muafaka mwezi Novemba.

Euro 40 zitatumika katika uwekezaji binafsi

Kiasi cha Euro bilioni 40 ya bajeti hiyo kitatumika kuinua uwekezaji binafsi katika sekta ya nishati, usafiri na mitandao ya digitali. Italia ilipambana kupinga mapendekezo ya Uingereza ya kubana matumizi huku Waziri Mkuu Mario Monti akiwa anajiandaa na uchaguzi baadaye mwezi huu, ambapo pia waziri mkuu wa zamani, Silvio Berlusconi, akiwa ametangaza kurejea katika ulingo wa siasa kwa ahadi ya kuongeza ajira na kusaidia kukuza uchumi wa nchi hiyo.

Kwa upande wake, Rais Francois Hollande wa Ufaransa alisema asingeweza kukubaliana na bajeti ya Umoja huo iwapo itapuuzia suala la kilimo na ukuaji wa uchumi. Suala jingine linalopaswa kutatuliwa kwa sasa ni mfumo wa kurejesha fedha, ambao unapunguza michango ya bajeti ya Umoja wa Ulaya ya Uingereza na wachangiaji wenzake wakuu, Austria, Ujerumani, Uholanzi na Sweden.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE
Mhariri:Josephat Charo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com