1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wakosa mwafaka wa kufungua mipaka kwa wageni

27 Juni 2020

Mataifa ya Umoja wa Ulaya jana yameshindwa kufikia makubaliano juu ya orodha ya nchi zilizo salama ambazo raia wake wangeweza kuruhusiwa kuanza kusafiri ndani na nje ya kanda hiyo kuanzia mwezi Julai.

https://p.dw.com/p/3eQ26
PK EU-China-Gespräche
Picha: picture-alliance/dpa/European Council/D. Pignatelli

Mabalozi wa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya walikutana mjini Brussels jana kutayarisha mwongozo wa kuruhusu baadhi ya raia wa mataifa kadhaa duniani kuanza kuingia tena kwenye mataifa ya kanda hiyo bila ya masharti ya kukaa karantini.

Hata hivyo wanadiplomasia hao wameomba muda zaidi wa kushauriana na serikali za mataifa yao kabla ya kufikia uamuzi wa orodha ya nchi 10 hadi 20 zilizopendekezwa na uamuzi unatarajiwa kutolewa baadae hii leo.

Duru kutoka mjini Brussels zimesema orodha ya mataifa iliyowasilishwa kwa mabalozi hao haikuzujumuisha Marekani, Brazil wala Urusi, nchi ambazo bado zina kiwango kikubwa cha maambukizi ya virusi vya corona.

Kulingana na maafisa wawili wa Marekani abiria kutoka Marekani wataruhusiwa kusafiri ikiwa watatimiza masharti kadhaa ikiwemo kupita katika vituo vya ukaguzi wa joto la mwili.

Uondoaji vizuizi vya ndani bado ni changamoto 

EU-Projekt Neue Webplattform Re-open EU
Picha: European Union, 2020

Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya ilitoa ushauri kwa kanda hiyo kuondoa kwanza vizuizi vya mipaka ya ndani na kisha baadae kuanza kufungua milango kwa wageni kutoka nje ya kanda hiyo.

Hata hivyo, hatua ya kwanza haikufanikiwa kama ilivyoanishwa kwenye mpango.

Ugiriki inawalazimisha wageni wote kutoka mataifa kadhaa ya kanda ya Umoja wa Ulaya kufanyiwa vipimo vya ugonjwa wa COVID-19 na kujiweka karantini hadi matokeo yatakapotolewa.

Jamhuri ya Czech imesema haitoruhusu watalii kutoka Ureno, Sweden na sehemu fulani za Poland kuingia nchini humo.

Kwa sehemu kubwa mataifa ya kanda hiyo yanakubaliana kuwa yanapaswa kuruhusu wageni kutoka mataifa yenye viwango sawa au vizuri zaidi vya mafanikio ya kudhibiti ugonjwa wa COVID-19 lakini kuna wasiwasi juu ya vipi Umoja wa Ulaya utaweza kuhakiki hatua za mataifa hayo katika kukabiliana na janga hilo au kuaminika kwa taarifa zinazotolewa na serikali zake.

Kwa mujibu wa Wakala wa Kupambana na Kuzuia Magonjwa wa Umoja wa Ulaya mataifa  kadhaa kama Tanzania, Turkmenistan na Lao hayajaripoti visa vyovyote vya maambukizi katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Kwa kuzingatia taarifa za taasisi hiyo katika kipindi cha wiki mbili zilizopita mataifa kadhaa yamefikia kiwango kibaya kabisa cha maambukizi kuliko Umoja wa Ulaya.

Mataifa hayo yanajumuosha Marekani, Mexico, Brazil na sehemu kubwa ya Amerika ya Kusini, Urusi, Afrika Kusini na Saudi Arabia.

Afrika Kusini yalegeza zaidi marufuku za COVID-19 

Süfafrika Johannesburg | Covid-19 Impfstoff Tests beginnen
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Sibeko

Katika hatua nyingine Afrika Kusini imesema itaruhusu kufunguliwa tena kwa mikahawa na kumbi za starehe kuanzia Jumatatu inayokuja katika hatua ya hivi karibuni kabisa ya kulegeza vizuizi vya kukabiliana na virusi vya corona licha ya kuongezeka visa vya maambukizi nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na waziri wa Utalii Mmamoloko Ngubane imesema uamuzi huo umefikiwa ili kunusuru sekta ya utalii na biashara baada ya takwimu mpya kuonesha kiasi nafasi 600, 000 za ajira zinaweza kupotea iwapo vizuizi vilivyopo vitaendeela hadi mwezi Septemba.

Ngubane amesema kumbi zote za starehe zitaruhusiwa kufanya kazi kwa asilimia 50 ya uwezo wake huku mikahawa na vituo vya kuuza chakula itaruhusiwa kupokea wateja lakini uuzaji wa pombe bado umepigwa marufuku.

Hadi sasa Afrika Kusini imerikodi zaidi ya visa 118,000 vya maambukizi ya virusi vya corona pamoja na vifo 2,200 huku idadi ya maambukizi mapya ilipanda ghafla siku ya Alhamisi na kufikia visa 6500 kwa siku kutoka visa 1000 mwezi Aprili.