1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wakataa kuingilia suala la Catalonia

Isaac Gamba
20 Oktoba 2017

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekataa kusaidia kuutatua mgogoro wa jimbo la Catalonia wakisema ni wajibu wa serikali kuu ya mjini Madrid na Barcelona  kutafuta suluhu ya mkwamo huo wa kisiasa.

https://p.dw.com/p/2mEK7
Belgien EU-Gipfel
Picha: Reuters/V. Mayo

Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk aliwaeleza waandishi wa habari wakati wa mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels  kuwa suala la Catalonia haliko katika ajenda za mkutano huo.

" Sisi sote tuna mawazo yetu, hisia  na tathimini zetu lakini kwa taarifa tu hakuna nafasi ya Umoja wa Ulaya kuingilia mgogoro huo na nchi wanachama wanaelewa fika kuwa hakuna nafasi hiyo".  Alisema Tusk.

Hayo yanajiri mnamo wakati rais wa jimbo la Catalonia  Carles Puigdemont akipuuza muda wa mwisho aliopewa na serikali ya mjini Madrid  kubatilisha nia  yake ya  kutaka kutangaza uhuru wa jimbo hilo ambapo siku tatu alizopewa kufanya hivyo zimemalizika asubuhi ya leo na badala yake kiongozi huyo amemuandikia barua waziri mkuu Mariano Rajoy akitishia kutangaza uhuru wa jimbo la Catalonia.

"Puigdemont amesema " Iwapo serikali ya mjini Madrid itaendelea kukataa majadiliano pamoja na kuzima suala hili basi bunge la Catalonia litaendelea" alisema Puigdemont.

Rajoy anapanga kutumia ibara ya 155 ya katiba ya mwaka 1978 ambayo inamruhusu kuchukua mamlaka  ya jimbo lolote iwapo itabainika limevunja sheria.

Kakao maalumu cha baraza la mawaziri kimepangwa kufanyika Jumamosi ili kuandaa orodha ya hatua kwa ajili ya kuidhinishwa na seneti

Serikali ya Uhispania yapanga kumpokonya madaraka Puigdemont

Spanien Carles Puigdemont Premier der Regionalregierung
Kiongozi wa jimbo la Catalonia Carles PuigdemontPicha: Reuters/A. Gea

Hatua zinazofikiriwa ni pamoja na kumuondolea madaraka ya urais kiongozi wa jimbo la Catalonia Carles Puigdemont, kulipokonya jimbo hilo madaraka ya kusimamia masuala ya elimu na shule, kuitisha uchaguzi mpya, kuvunja bunge la jimbo hilo pamoja na kudhibiti vyombo vya habari vya umma  vinavyoonekana kuwa njia inayotumiwa  na jimbo hilo kutangaza nia yake ya kutafuta uhuru wa jimbo hilo.

Hadi sasa Puigdemont ametoa mwito wa kufanyika majadiliano kati ya uongozi wa jimbo hilo na serikali ya mjini Madrid pamoja na wapatanishi wa kimataifa.

Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akizungumzia suala hilo mjini Brussels amesema kuwa wanaunga mkono msimamo wa serikali ya Uhispania  na kuongeza kuwa ana mataumaini suluhu itapatikana kwa kuzingatia katiba  ya Uhispania huku Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte akisema  hilo ni suala la ndani kauli iliyoungwa mkono na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliyefanya kikao cha faragha na  na Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy pembezoni mwa mktano huo wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya.

Spanien Mariano Rajoy im Parlament
Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano RajoyPicha: Reuters/J. Medina

Kwa mujibu wa mwanadiplomasia wa Ufaransa aliezungumza na shirika la habari la Reuters Macron  alisema ana imani kubwa na Rajoy katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo wa kisiasa.  Naye Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema mgogoro wa Catalonia ni suala la ndani la Uhispania na kukosoa undumilakuwili wa nchi za magharibi kwa kuunga mkono suala la Kosovo na kujiweka kando katika masuala mengine  kama hayo.

Wakazi wa Catalonia wapatao milioni 7.5 wamegawanyika kuhusiana na hoja hiyo ya kujitenga  ambapo wapiga kura wengi wanaopinga uhuru wa wa jimbo hilo walijiweka kando na kura hiyo ya maoni ambayo ilitangazwa kuwa ni batili na mahakama ya kikatiba ya Uhispania.

Wakati huohuo viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Brussels kujaribu kutafuta njia za kuharakisha mazungumzo yanayohusiana na mchakato wa Uingereza kujiondoa kwenye Umoja huo ujulikanao kama Brexit. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema hana mashaka yoyote   na anaimani Umoja wa Ulaya na Uingereza watapata mafanikio katika suala hilo la Brexit.

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema mazingira yanayowekwa na viongozi hao wa Umoja wa Ulaya kuhusiana na suala hilo yatasaidia kuwezesha kusonga mbele kwa mchakato huo wa Brexit.

Mwandishi: Isaac Gamba/dw/rtre/ape

Mhariri   : Mohammed Abdul-Rahman