Umoja wa Ulaya waitisha kikao maalum kujadili matatizo ya Kampuni ya General Motors | Masuala ya Jamii | DW | 06.03.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Umoja wa Ulaya waitisha kikao maalum kujadili matatizo ya Kampuni ya General Motors

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kuitembelea kampuni ya Opel Machi 31

Günter Verheugen, kamisha wa Umoja wa Ulaya anayehusika na viwanda

Günter Verheugen, kamisha wa Umoja wa Ulaya anayehusika na viwanda

Halmashauri ya Umoja wa Ulaya imependekeza kufanyika mazungumzo ya dharura ya nchi wanachama wa umoja huo zilizo na viwanda vya kampuni ya kutengeza magari ya General Motors ili kuratibu msaada kwa kampuni hiyo ya Marekani.

Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na maswala ya viwanda, Günter Verheugen, amesema nchi wanachama wa umoja huo zenye viwanda vya kampuni ya magari ya General Motors zinatakiwa kukutana kuzungumzia mikakati ya pamoja ya kukabiliana na matatizo ya kiuchumi yanayoikabili kampuni hiyo.

"Nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya ambazo zina viwanda vya kampuni ya kutengeza magari ya General Motors zinatakiwa kufanya mkutano maalum ili kujadiliana kwa pamoja kuhusu hatua za kukabiliana na hali hii."

Bwana Verheugen pia amesema angependa kujua nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Ulaya zilizo na viwanda vya kampuni ya General Motors zinatafakari kuchukua hatua gani. Ameongeza kuwa hatua zote zitakazochukuliwa barani Ulaya zinatakiwa ziratibiwe kwa pamoja na kwamba kila nchi haipaswi kujichukulia hatua zake peke yake.

Mazungumzo hayo hayazijumulisha nchi zenye viwanda vya kampuni ya General Motors, zikiwemo Ubelgiji, Uingereza, Ujerumani, Uhispania, Ureno na Sweden, bali pia zile zenye matawi ya kampuni hiyo.

Ujumbe wa kampuni ya General Motors umeondoka Marekani hii leo kuelekea hapa Ujerumani.

Matatizo yanayoikabili kampuni ya General Motors nchini Marekani yamesababisha athari kubwa katika tawi lake la Ulaya la Opel ambalo linaendesha shughuli zake nyingi hapa Ujerumani likiwa na viwanda vinne. Kufilisika kwa kampuni ya Opel hapa Ujerumani kutasababisha kupotea kwa nafasi takriban 400,000 za ajira barani Ulaya.

Kampuni ya General Motors ina wafanyakzi 55,600 barani Ulaya wakiwemo 26,000 katika kiwanda cha Opel nchini Ujerumani. Kampuni ya vyuma ya Ujerumani AG Metal imeliambia gazeti la Berliner Zeitung kwamba kufilisika kwa kampuni ya Opel kutakuwa na athari kubwa katika mauzo ya vipuri vya magari.

Akizungumzia kuhusu hali ngumu inayoikabili kampuni ya General Motors na vipi inavyoathiri shughuli za kapuni ya Opel hapa Ujerumani, waziri wa uchumi wa Ujerumani, Karl-Theodor zu Guttenberg anasema, "Tulikubaliana kwa mapana kuhusu wazo kwamba hali inayoikabili kampuni mama ya General Motors nchini Marekani, haiwezi kusaidia kufaulu kujenga uaminifu, kwamba hali itaendelea kubakia ya kutoeleweka: haijulikani safari inaelekea wapi."

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ataitembelea kampuni ya Opel Machi 31. Msemaji wa kiongozi huyo amesema huenda kansela Merkel akatangaza uamuzi wa kuikoa kampuni hiyo ya kutengeza magari.

Ziara ya kansela Merkel katika kiwanda kikuu cha Opel kilichoko mjini Ruesselsheim karibu na mji wa Frankfurt, ilikuwa imepangwa kwa muda na haihusiani na mpango wa kuinusu kampuni hiyo. Lakini gazeti la Bild limeripoti huenda kansela Merkel akaitumia ziara hiyo kutangaza msaada wa serikali kwa kampuni ya Opel.

Kampuni ya General Motors barani Ulaya imewasilisha mapendekezo ya mageuzi yanayojumulisha yuro bilioni 3.3 msaada wa serikali ya Ujerumani na nchi nyingine za Ulaya.

 • Tarehe 06.03.2009
 • Mwandishi Charo, Josephat/AFP
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/H6mR
 • Tarehe 06.03.2009
 • Mwandishi Charo, Josephat/AFP
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/H6mR
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com