1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wahusika katika unyanyasaji wa wahamiaji

Zainab Aziz
12 Desemba 2017

Amnesty International katika ripoti yake imezilaumu nchi za Umoja wa Ulaya kwa kushiriki katika unyanyasaji wa wahamiaji nchini Libya kwa sababu ya kufumbia macho ukatili wa walinzi wa pwani ya.

https://p.dw.com/p/2pBrl
Libyen Migranten und Flüchtlinge auf einem Schlauchboot
Picha: Getty Images/AFP/A. Solaro

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika hilo iliyotolewa leo, serikali za Ulaya moja kwa moja zimeshiriki katika matendo hayo ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Libya kutokana na nchi hizo kuendelea kutoa misaada kwa mamlaka nbalimbali za nchini Libya ambazo mara nyingi hushirikiana na watu wanaofanya biashara haramu ya kuuza watu na pia mamlaka hizo zinahusika na vitendo vya kuwanyanyasa wakimbizi na wahamiaji.

Wahamiaji kutoka Afrika kwenye bahari ya Mediterrania (picture-alliance/AP/S. D
Wahamiaji kutoka Afrika kwenye bahari ya MediterraniaPicha: picture-alliance/AP/S. Diab

Amnesty International katika ripoti yake imesema kuwa ina ushahidi unaoonyesha walinzi hao wa pwani ya Libya wakipokea rushwa kutoka kwa watu wanaofanya biashara haramu ya kuwasafirisha watu kinyume cha sheria ili kuziruhusu mashua zinazobeba wahamiaji kuondoka kutoka kwenye pwani ya Libya kwenda Ulaya.

Taasisi hiyo ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu imeelezea kwamba takriban watu elfu 20 bado wanazuiwa, wanateswa, kufanyishwa kazi kwa lazima, wanatishiwa na kuyang'anywa fedha zao na wakati mwingine wanauawa kinyama.

Shirika hilo limetolea mfano wa tukio la tarehe 6 Novemba ambapo kulizuka vurugu kati ya walinzi wa pwani na maafisa wa shirika moja la kutoa misaada la Ujerumani la Sea- Watch ambapo wahamiaji wapatao watano walikufa. Serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa yenye makao yake katika mji wa Tripoli imesema Libya na Italia zitaunda tume ya pamoja ya kupambana na wafanyabiashara haramu ya kuuza watu na pia kukabiliana na uhamiaji haramu.

Aliyekuwa kiongozi wa Libya Muammar Gadaffi
Aliyekuwa kiongozi wa Libya Muammar GadaffiPicha: AP

Mitandao ya wafanyabiashara haramu ya kuuza binadamu inaendelea kukua katika nchini Libya inayokabiliwa na machafuko yaliyozuka tangu kung'olewa madarakani aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu Muammar Gaddafi mnamo mwaka 2011.

Mkurugenzi wa shirika hilo la kutetea haki za bindamu tawi la Ulaya, John Dalhuisen amesema nchi za Ulaya zinaendelea kutoa msaada kwa mamlaka ya Libya kwa ajili ya kusaidia kumaliza shughuli za kuwasafirisha watu kwa njia ya baharini na pia kuendesha kampeni ya kuhakikisha kuwa vijana wanabakia katika nchi zao, lakini kwa bahati mbaya serikali hizo za Ulaya hazitambui kama fedha hizo zinachangia katika uvunjifu wa haki za binadamu na hivyo kuzifanya serikali hizo kuwa ni washiriki katika vitendo hivyo viovu.

Serikali za Ulaya zimewapa mafunzo na vifaa walinzi wa pwani ya Libya, hasa wa Italia, kwa ajili ya kuzuia wimbi la wahamiaji wanaokwenda barani Ulaya.

Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE/APE/DPAE/

Mhariri: Grace Patricia Kabogo