Umoja wa Ulaya na Urusi zaanza mazungumzo ya ushirikiano | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Ulaya na Urusi zaanza mazungumzo ya ushirikiano

Yatajikita katika masuala ya nishati na ulinzi

Mkuu wa tume ya Ulaya Jose Manuel Barroso aonya mradi wa bomba la gesi kutoka Urusi hadi Ujerumani usihatarishe mazingira

Mkuu wa tume ya Ulaya Jose Manuel Barroso aonya mradi wa bomba la gesi kutoka Urusi hadi Ujerumani usihatarishe mazingira

Umoja wa Ulaya pamoja na Urusi zimeanza mazungumzo ijumaa ambayo yanahusu ushirikiano mpya wa kiuchumi na kisiasa.

Umoja wa Ulaya unatumaini kuwa uhusiano huu mpya utatoa ufafanuzi zaidi wa jinsi ya kupata mafuta na gesi kutoka Urusi.

Mkutano huu kati ya Urusi na Umoja wa Ulaya ambao unafanyika mjini Brussels Ubelgiji ndio wa kwanza wa aina hiyo wakati huu ambao utagusia sekta mbalimbali.Miongoni mwa sekta hizo ni Nishati pamoja na elimu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka uongozi wa Umoja huo ya tume ya Ulaya,pande zote mbili zitamulika kile kilichoitwa,masuala ya kupewa kipaumbele katika mazungumzo pamoja na ajenda, na vilevile kuweka ratiba ya mazungumzo.

Mkataba uliopo baina ya pande hizo mbili wa miaka 10 uliotiwa saini mwaka wa 1997, licha ya kupitwa na wakati lakini baado unatumika ikisubiriwa kupata mwingine mpya.

Hata hivyo umepoteza makali yake kutokana na utajiri mpya wa mafuta na gesi wa Urusi pamoja na msimamo usiotetereka wa masuala ya kigeni ya Urusi.

Mazungumzo haya ambayo yako katika kiwango cha ubalozi yamekuja wiki moja tu baada ya viongozi wa Umoja wa Ulaya kukutana kwa mazungumzo na kiongozi mpya wa Urusi Dmitry Medvedev. Mkutano wao ulifanyika katika mji mmoja unaopatikana katika eneo lenye mafuta mengi la Siberia.

Na umeelezwa kama mwanzo wa enzi mpya ya uhusiano mzuri kati ya Urusi na majirani zake wa Ulaya.

Lakini mazungumzo yaliyoanza leo,ambayo yana nia ya kupatikana kwa kanuni za kisheria ambazo zitafuatwa katika ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Urusi katika karibu nyaja zote, yanatarajiwa kuwa magumu.

Pande zote mbili zinatofautiana kuhusu mwelekeo wa mkataba mpya.Urusi inataka mpango jumla ambao unafuata ule uliomalizika mwaka jana.Nao Umoja wa Ulaya kwa upande mwingine unasisitiza kuwepo mkataba mpana zaidi ukiwa na maelezo rasmi kuhusu masuala ya nishati na usalama.

Umoja wa Ulaya unataka utawala wa Moscow ufungue milango ya sekta yake ya nishati kwa wawekezaji wa umoja wa huo.

Urusi kwa upande wake imetaka makampuni yake nayo yapewe nafasi ya kuwekeza katika mitandao ya usambazaji wa mafuta na gesi barani Ulaya.

Hata hivyo pande hizo mbili tayari zimekubaliana kuuunga mkono mradi mpya wa bomba kutoka bahari ya Baltic hadi hapa Ujerumani.Mradi huo ambao tayari umeshazusha sintofahamu miongoni mwa mataifa ya umoja wa Ulaya utakuwa wakusafirisha gesi.

Rais Medvedev amesema kuwa mradi huo ni wa kibiashara tu ambao umepakwa matope kwa sababu za kisiasa.

Sharti pekee la Umoja wa Ulaya kuhusu mradi huo limetoka kwa mkuu wa umoja huo,Jose Manuel Barroso.Yeye ameomba tu kuwa bomba hilo lifuate kiwango cha kulinda mazingira.

 • Tarehe 04.07.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EWJA
 • Tarehe 04.07.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EWJA
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com