Umoja wa Ulaya na China zajadili biashara na uwekezaji | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.09.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Ulaya na China zajadili biashara na uwekezaji

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na maafisa waandamizi wa Umoja wa Ulaya wamefanya mazungumzo na rais wa China Xi Jinping, wakijadili masuala ya biashara, uwekezaji na kujenga imani juu ya masuala magumu ya kisiasa.

Merkel ambaye taifa lake linashikilia urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya, alihudhuria mkutano huo kwa njia ya vidio, sambamba na rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel, rais wa Halmashauri ya muungano huo Ursula von der Leyen na mkuu wa sera za kigeni Josep Borrel.

Mazungumzo kati ya pande hizo mbili zilizo na nguvu kubwa kiuchumi duniani na wafanyabiashara, ilikuwa ni fursa kwa Brussels na Beijing kuchukua usukani wa mahusiano yao huku Umoja wa Ulaya ukitaka kujikita zaidi katika masuala ya kiuchumi, mageuzi ya shirika la kimataifa la biashara WTO, mabadiliko ya tabia nchi na janga la virusi vya corona.

Kabla ya kufanyika mazungumzo ya kibiashara, pande mbili zilitia saini mkataba wa kulinda vyakula na vinjwaji vinavyosafirishwa kwa kila mmoja. China ilikuwa ni soko la tatu kwa bidhaa za chakula za Umoja wa Ulaya mwaka 2019, zilizokuwa na thamani ya euro bilioni 14.5.

Umoja wa Ulayaunaiona China kama "mpinzani wa kimfumo" anayetoa fursa nzuri lakini pia akionyesha changamoto nyingi. Janga la virusi vya corona pia limeibua changamoto mpya, haswa kile Brussels inachokitizama kama kampeni iliyoanzishwa na China ya kutotoa taarifa juu ya ugonjwa ambao unaweza kuweka maisha ya watu hatarini.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel aliandika katika ukurasa wa twitter akisema kuwa "ni wakati wa kuchukua hatua za kweli za kushughulikia kukosekana kwa usawa na kuonyesha uongozi wa ulimwengu".

EU-China-Gipfel zu Markenschutz

Mkutano wa Umoja wa Ulaya na rais wa China

Mitazamo ya umoja wa Ulaya kuelekea Beijing imekuwa migumu kutokana na janga la virusi vya corona, ambalo wanasayansi wanaamini lilianzia China na kwasababu ya sheria mpya ya usalama huko Hong Kong ambayo mataifa ya magharibi yanadai kuwa inabinya haki za msingi.

Umoja wa Ulaya unataka uwajibikaji zaidi wa China katika suala la mabadiliko ya tabia nchi kwakuwa taifa hilo ndilo linaongoza kwa uchafuzi wa hali ya hewa duniani. Pande hizo mbili zimekuwa zikijaribu kufikia makubaliano ya uwekezaji kufikia mwishoni mwa mwaka huu, ili kuweza kuyapa uwanda mpana makampuni ya Ulaya katika soko la China na kuzuia Umoja wa Ulaya kuongeza ulinzi wa biashara.

"Tunatumai Umoja wa Ulaya utazingatia tena kwa uangalifu kuitizama China kama "mshindani wa kimfumo", ameandika mwanadiplomasia wa China katika muungano huo akimaanisha msimamo wa Ulaya kwamba Beijing inakuwa mpinzani kuliko mshirika.

Umoja wa Ulaya pia unakusudia kutilia mkazo wasiwasi juu ya mvutano katika bahari ya Kusini ya China na kufanya mazungumzo baadae mwaka huu yanayohusu haki za binadamu.