Umoja wa Ulaya kuzungumza na Uturuki | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.07.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Ulaya kuzungumza na Uturuki

Nchi za Umoja wa Ulaya zimekubaliana kuongeza juhudi zao ili kutuliza mvutano na Uturuki kwa njia ya mazungumzo, huku pia zikiweka hatua mpya za adhabu endapo Uturuki haitaitikia mwito.

Mawaziri wa mambo ya nje wa EU wakutana mjini Brussels.

Mawaziri wa mambo ya nje wa EU wakutana mjini Brussels.

Nchi za Umoja wa Ulaya zimekubaliana kuongeza juhudi zao ili kutuliza mvutano na Uturuki kwa njia ya mazungumzo, huku pia zikiweka hatua mpya za adhabu endapo Uturuki haitaitikia mwito. Umoja wa Ulaya umekuwa ukiandaa pia vikwazo dhidi ya China kufuatia sheria mpya ya usalama kuhusu Hong Kong.

Katika mkutano wa mawaziri 27 wa nchi za nje wa umoja huo, uliofanyika mjini Brussels suala la Uturuki lilipewa kipaumbele. Mataifa ya Umoja wa Ulaya yameghadhabishwa na Uturuki kuhusu masuala kadhaa, ikiwemo utafiti kuhusu uchimbaji wa mafuta na gesi katika eneo linalozozaniwa pwani ya Cyprus, kuingilia katika machafuko ya Libya pamoja na hatua ya taifa hilo kuibadili makumbusho ya Hagia Sophia na kuifanya msikiti. Baada ya mkutano wao, mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell alisema mawaziri wamemtaka kutafuta njia kadhaa za kutuliza mvutano na wapate suluhisho kuhusu masuala tete yanayozidi kuuwekea shinikizo uhusiano wao na Uturuki.

''Tutaendelea kufuata namna itakavyowezesha kupunguza hali ya wasiwasi. Na kwa hakika kuibana Ugiriki, katika eneo la maji linalozozaniwa nchini humo huenda likawa suala linaloweza kuongeza wasiwasi. Na kwa upande mwingine, wakati huo huo tutaandaa mapendekezo kuhusu hatua zaidi zinazoweza kuchukuliwa katika kukabiliana na changamoto zinazotukabili zinazosababishwa na hatua za Uturuki'',alisema Borrel.

EU yatishia pia vikwazo dhidi ya China

 Uturuki kuibadili makumbusho ya Hagia Sophia na kuifanya msikiti.

Uturuki kuibadili makumbusho ya Hagia Sophia na kuifanya msikiti.

Borrel aliyefanya ziara wiki iliyopita mjini Ankara kwa mazungumzo na mawaziri wa Uturuki, amelezea nia ya kuweko na suluhisho la mvutano kupitia mazungumzo, lakini kuna baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ambazo zinataka Uturuki ichukuliwe hatua kali, zikiwemo vikwazo.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan alisema jana kwamba suala la msikiti wa Hagia Sophia ni suala la kitaifa na la ndani na mataifa mengine wajibu wao ni kuheshimu maamuzi yaliyochukuliwa na taifa huru.

Licha ya changamoto baina ya Umoja wa Ulaya na Uturuki, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas alisema kwamba Uturuki imebaki kuwa na umuhimu wa kimkakati kwa Umoja wa Ulaya na ni bora kuendelea kuweko na mazungumzo.

Mawaziri wa Umoja wa Ulaya pia walijadili uwezekano wa vikwazo dhidi ya China kuhusu sheria mpya ya usalama huko Hong Kong. Lakini baadhi ya wanadiplomasdia wanasema hakuna uwezekano wa vikwazo vya kiuchumi.

Kama nchi kadhaa za magharibi, Umoja wa Ulaya umelaani hatua ya bunge la China la kupitisha sheria ya kiusalama kuhusu Hong Kong.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com