Umoja wa ulaya kutuma wanajeshi wa kulinda amani mashariki mwa Chad. | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.07.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa ulaya kutuma wanajeshi wa kulinda amani mashariki mwa Chad.

Ni jibu kwa mashambulio yanayofanywa na wanamgambo wanaovuka mpaka wa nchi hiyo na Sudan dhidi ya raia wasio na hatia.

Wakimbizi kutoka Sudan nchini Chad

Wakimbizi kutoka Sudan nchini Chad

Kiasi ya wakimbizi 230,000 kutoka jimbo la magharibi mwa Sudan la Darfur na 170,000 waliolazimika kutawanyika kutokana na machafuko ndani ya Chad wako katika makambi mashariki mwa Chad, eneo lenye miundo mbinu duni.

Pamoja na maafa yanayotokana na ukosefu wa liche bora, wakimbizi hao wamekua katika hali ya hofu kutokana na hujuma zinazofanywa na wanamgambo wa Janjaweed wanaoungwa mkono na serikali ya Sudan, na ambao wamekua wakifanya vitendo vya mauaji dhidi ya raia. Hali ya usalama imezidi kuwa mbaya kutokana na ujambazi na machafuko ya kikabila ndani ya Chad yenyewe.

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa ulaya watakutana mjini Brussels tarehe 23 na 24 ya mwezi huu, wakitarajiwa kuidhinisha mpango wa kutuma wanajeshi wa kusimamia amani mashariki mwa Chad. Ujumbe huo huenda ukawahusisha wanajeshi 3,000 pamoja na shughuli za polisi ,wakihusika kiasi ya watumishi 1,000 .

Katika hatua ya mwanzo ni wanajeshi wa nchi za ulaya tu watakaohusika, ingawa inatarajiwa kwamba jukumu la kikosi hicho litakabidhiwa umoja wa mataifa baada ya mwaka mmoja. Mkuu wa idara inayosimamia shughuli za amani Jean-Marie Guehenno alikua na mazungumzo juma lililopita na maafisa wa kibalozi mjini Brussels, kuhusiana na baadhi ya mikakati inayozingatiwa.

Alan Deletroz kutoka taasisi ya kimataifa inayohusika na migogoro, amesema kwamba lakuzingatiwa ni kuhakikisha kwamba wanajeshi kutoka Chad na Ufaransa hawapaswi kuwa sehemu kubwa katika kikosi hicho. Akaongeza kwamba ametiwa moyo baada ya kufahamika kwamba ni karibu nusu tu ya wanajeshi watatoka Ufaransa , mkoloni wa zamani wa Chad.

Kinyume chake , katika harakati za kwanza kabisa za kusimamia amani za umoja wa ulaya barani Afrika-wakati wanajeshi wake walipopelekwa mkoa wa Ituri katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, wengi wa wanajeshi walitokea Ufaransa.

Ufaransa imekua mtoaji mkubwa wa msaada wa kijeshi kwa utawala rais wa Chad Idris Deby aliingia madarakani katika mapinduzi ya kijeshi 1991. Wakati wapizani wake walipojaribu kumuangusha mwaka jana katika shambulio kwenye mji mkuu Ndjamena, Ufaransa ilimsaidia kijeshi.

Afisa mmoja wa umoja wa ulaya anayehusika na maswala ya usalama, alisema kikosi cha umoja wa ulaya kinatarajiwa kupelekwa Chad kabla ya mwisho wa mwaka huu, lakini majukumu yake bado hayajafafanuliwa.

Mnamo mwezi huu shirika la haki za binaadamu Human rights watch, lilitoa taarifa juu ya janga linalowakabili watoto, kutokana na mgogoro ndani ya Chad na pamoja na wakimbizi kutoka jimbo la Sudan la Darfur.

Sambamba na hayo mtindo wa kuwaingiza watoto katika mapigano umeongezeka ndani ya jeshi la taifa la Chad na pia kundi la waasi-United Front for Change-ikisemekana watoto wadogo hadi miaka minane wanatumiwa katika mapigano, kama wapishi na walinzi katika vituo vya ukaguzi.

Pamoja na hayo mtaalamu wa maswala ya Afrika katika Jumuiya ya kijerumani kwa ajili ya watu walio hatarini Ulrich Delius, anasema mtoto mmoja katika kila wawili chini ya umri wa miaka mitano katika makambi ana tatizo la liche bora na majeshi ya usalama nchini Chad yanashindwa kusambaza chakula cha msingi. Akaongeza kuwa endapo hatua za usalama wa wakimbizi hazitoboreshwa haraka, kuna kitisho kikubwa , na kwamba sio tu kwa maelfu ya wakimbizi watafariki, lakini Chad itatumbukia katika machafuko na ukosefu wa utaratibu wa utawala.

 • Tarehe 18.07.2007
 • Mwandishi Mohammed Abdul-Rahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHAs
 • Tarehe 18.07.2007
 • Mwandishi Mohammed Abdul-Rahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHAs

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com