1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kutoa euro milioni 440 kwa Palestina

17 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CcsV

Umoja wa Ulaya umeahidi msaada wa euro milioni 440 kwa Wapalestina kwenye mkutano wa wafadhili uliofanyika leo mjini Paris, Ufaransa.

Waziri mkuu wa mamlaka ya Palestina, Salam Fayyad, ameomba rasmi euro bilioni 3.85 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, ameuambia mkutano wa mjini Paris kwamba bila msaada wa kifedha maeneo ya Ukanda wa Gaza na ukingo wa magharibi wa mto Jordan, yatakabiliwa na janga kubwa la kibinadamu. Rais Abbas amesema serikali yake itatumia baadhi ya fedha zitakazotolewa kuwasaidia wakaazi wa eneo la ukanda wa Gaza linalotawaliwa na chama cha Hamas.

Waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, ameziunga mkono juhudi za jumuiya ya kimataifa kutaka kuufua uchumi wa Palestina lakini akaonya hatakubali usalama wa Israel uvurugwe.

Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, amewataka viongozi wa Israel na Palestina watumie nafasi hii kuwa na amani.

´Tumieni nafasi hii nzuri kabisa kwa ajili ya kufikia amani. Msiiache nafasi hii ya kihistoria iwapite. Wakati wa amani umewadia. Hilo ndilo wanalolitaka wananchi wenu. Wapeni raia wa Isreal na Palestina zawadi maridhawa kabisa nayo ni amani.´

Mkutano wa siku moja wa mjini Paris unafuatilia maswala yaliyokubaliwa kwenye mkutano uliofanyika mwezi uliopita mjini Annapolis katika jimbo la Maryland nchini Marekani, uliolenga kufikia suluhisho la mataifa mawili ya Israel na Palestina.