1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi

24 Oktoba 2014

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameahidi kupunguza moshi wa sumu unaotoka viwandani kwa angalau asili mia 40 hadi ifikapo mwaka 2030-lengo likiwa kuongoza juhudi za kimataifa za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

https://p.dw.com/p/1DbWr
Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels.Picha: Carl Court/Getty Images

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameahidi kupunguza moshi wa sumu unaotoka viwandani kwa angalau asili mia 40 hadi ifikapo mwaka 2030-lengo likiwa kulifanya bara la Ulaya liwe mshika bendera wa dunia katika juhudi za kuinusuru dunia na mabadiliko ya tabia nchi.

Baada ya majadiliano moto moto yaliyodumu zaidi ya masaa kumi mjini Brussels, viongozi wa umoja wa ulaya wamefanikiwa kuweka kando hitilafu zao za maoni kuhusu namna ya kuyafikia malengo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuidhihirishia hadhara barani Ulaya,wanaweza kuwafikiana.

"Makubaliano ya baraza la Ulaya kuhusu sera ya nishati na mabadiliko ya tabia nchi yanalenga mbali kuliko makubaliano yoyote mengine ya aina hiyo ulimwenguni"" amesema rais wa baraza la Ulaya Herman van Rompuy anaetarajia angalao kumaliza mhula wake wa miaka mitano kwa kufikiwa makubaliano dhabiti.

Maridhiano yaliyofikiwa yanazungumzia kuhusu kupunguzwa kwa asili mia 40 moshi wa sumu unaotoka viwandani hadi ifikapo mwka 2030 ikilinganishwa na kiwango cha mwaka 1990.

Viongozi 28 wa taifa na serikali wamekubaliana pia kuhusu malengo mawili mengine:kuhakikisha fungu la nishati mbadala linafikia asili mia 27 pamoja na kupunguza matumizi ya nishati kwa asili mia 27 ikilinganishwa na mwaka 1990.

"Ni habari za kutia moyo kwa mazingira,kwa wananchi wa Ulaya,kwa afya na kwa mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi utakaofnyika Paris mwaka 2015" amesema Van Rompuy aliyehakikisha malengo hayo yatabuni nafasi za kudumu za kazi na kuchocchea mashindano ya kibiashara.

"Ulaya inaonyesha mfano mzuri" amesema rais Francois Hollande wa Ufaransa aliyejiuliza tunanukuu" kama nchi za ulaya zitashindwa kusikilizana vipi zitaweza kuzitanabahisha Marekani na China.

Ujerumani ilipendelea kiwango cha juu zaidi

Katika mkutano na waandishi habari kansela Angela Merkel wa Ujerumani anasema:"Tumepiga hatua muhimu mbele,tumejiwekea lengo litakalodhamini Ulaya inasalia kuwa mdau muhimu na mshirika muhimu katika majukumu ya siku za mbele katika kufikia makubaliano ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.Tumesema tunataka angalao asili mia 27 ya nishati mbadala,ikimaanisha na hili ni muhimu zaidi ,kwa Ujerumani hicho ni kiwango cha chini tulichoweka.Tungeweza kulenga kiwango cha juu zaidi lakini fikra ya maridhiano ndio chanzo cha kufikiwa kiwango cha asili mia 27."

EU Gipfel 24.10.2014 Merkel und Hollande
Kansela Angela Merkel(kulia) na rais Francois HollandePicha: Reuters/Christian Hartmann

Bunge la Ulaya ambalo katika masuala ya sera za mbadiliko ya tabia nchi lina usemi pia,limewataka viongozi wa taifa na serikali wa umoja wa ulaya malengo yaliyofikiwa katika kikao cha jana usiku kuamkia leo yatekelezwe kivitendo.

Juhudi za kupambana na Ebola pia zimejadiliwa

Mbali na mabadiliko ya tabia nchi viongozi wa mataifa 28 ya Umoja wa ulaya wameridhia pia kuchaguliwa Christos Stylianides kuwa mjumbe maalum wa Umoja huo atakaesimamia juhudi za kupambana na maradhi ya Ebola Afrika magharibi.Umoja wa Ulaya umeahidi kuzidisha hadi Euro bilioni moja kiwango cha misaada kwaajili ya kukabiliana na maradhi hayo hatari.

Ebolaforschung in Marburg
Utafiti wa maradhi ya Ebola katika maabara ya mjini Marburg nchini UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa/ Thomas Strecker

Mwandishi: Reigert,Bernd/Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Yusuf Saumu