1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya, China wapata mwafaka juu ya paneli

27 Julai 2013

Kamisheni ya Umoja wa Ulaya imetangaza kupatikana kwa mwafaka baina yake na China, juu ya mabishano kuhusu biashara ya paneli za umeme wa kutumia miale ya jua ambayo yalikaribia kusababisha vita vya kibiashara kati yao.

https://p.dw.com/p/19FDd
Paneli za nishati ya jua kutoka China
Paneli za nishati ya jua kutoka ChinaPicha: STR/AFP/Getty Images

Kamishna wa Umoja huo anayehusika na biashara Karel de Gucht amesema leo Jumamosi kuwa muafaka huo utasaidia kufikia urari wa kibiashara na utengamanao wa bei katika soko. Licha ya kupatikana kwa mwafaka huo lakini, China na Umoja wa Ulaya bado zinatofautiana juu ya biashara ya bidhaa nyingine kama vile mabomba ya chuma cha pua, vifaa vya mawasiliano, mvinyo na bidhaa za kemikali.

Pande hizo mbili ni muhimu kiuchumi duniani, na ni washirika na washindani wa kibiashara. Biashara kati ya Umoja wa Ulaya na China ilikuwa na thamani ya Euro bilioni 415, na China imejichumia faida ya ziada kutokana hasa na mauzo ya bidhaa zinazotengenezwa huko kama vile chuma cha pua na simu za kisasa aina ya iPhone, kwenye soko la Ulaya.

Karel De Gucht, Kamishina wa Umoja wa Ulaya kuhusu biashara
Karel De Gucht, Kamishina wa Umoja wa Ulaya kuhusu biasharaPicha: Reuters

Makubaliano ya kiutu uzima

Serikali ya China imeukaribisha mwafaka uliopatikana, ikisema umeonyesha busara na kujitolea kwa pande husika katika kutanzua mzozo uliokuwepo. Msemaji wa wizara ya biashara ya nchi hiyo Shen Danyang ameviambia vyombo vya habari kuwa China inaunga mkono uwazi katika ushirikiano wa kibiashara.

Aidha, Karel De Gucht amesema muafaka uliofikiwa unaweka kiwango cha chini cha bei ya paneli za nishati ya jua zinazouzwa barani Ulaya, na kuongeza kuwa wanayo imani kwamba kiwango hicho kitaweka usawa kwenye soko la paneli na kuganga majeraha ambayo yalisababishwa na mrundikano wa bidhaa hizo zilizoingizwa kutoka China.

Bei ya kutupa kwenye soko

Kufuatia miezi kadhaa ya malumbano, mwezi Juni Umoja wa Ulaya uliweka sheria ya dharura, ambayo ingesababisha ongezeko la asilimia 47 kwa paneli kutoka China, iwapo mwafaka usingepatikana ifikapo tarehe 6 Agosti. De Gucht amedai kuwa kabla ya mwafaka, paneli kutoka China zilikuwa zinauzwa kwa bei ya kutupwa, ambayo ingeyafukuza makampuni ya Ulaya kwenye soko, na kusababisha upotevu wa nafasi nyingi za ajira.

China imeshutumiwa kuziuza paneli zake kwa bei inayoyafukuza sokoni makampuni ya Ulaya
China imeshutumiwa kuziuza paneli zake kwa bei inayoyafukuza sokoni makampuni ya UlayaPicha: Reuters

Kwa mujibu wa takwimu za China, nchi hiyo iliuza barani Ulaya paneli za nishati ya jua zenye thamani ya dola bilioni 35.8 mwaka 2011, hiyo ikiwa zaidi ya asilimia 60 ya mauzo yote ya bidhaa hizo kwenye soko la Ulaya. Wakati huo huo, China iliagiza kutoka Ulaya, paneli zenye thamani ya dola bilioni 7.5 tu.

Kamishna wa biashara wa Umoja wa Ulaya De Gucht, amesema baada ya muafaka uliopatikana, utaondoa kutolingana huko kwenye soko la biashara. Ripoti iliyotolewa leo kuhusu muafaka uliopatikana haikutaja kiwango cha chini kilichokubaliwa, lakini taarifa zilizotolewa mapema wiki hii zilisema kuwa kiwango hicho kitakuwa senti 57 za dola kwa kila wati ya nishati inayotengenezwa na paneli inayouzwa.

Makubaliano haya hayataanza kutekelezwa kabla ya kuidhinishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/DPAE

Mhariri:Caro Robi