1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa: Watu 800,000 Gaza hawana maji safi

22 Mei 2021

Umoja wa Mataifa umesema mbali na uharibifu wa makazi na majengo mengi muhimu, raia wa Ukanda wa Gaza hawana maji safi baada ya siku 11 za mashambulizi.

https://p.dw.com/p/3toQn
Israel - Palästina I Gaza Konflikt
Picha: AFP via Getty Images

Umoja wa Mataifa umesema watu wapatao 800,000 katika eneo la Gaza hawana maji safi , na karibu asilimia 50 ya njia za maji zimeharibiwa na mashambulizi ya hivi karibuni.

Ikinukuu wizara ya kazi na makazi ya Gaza, ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imesema makazi ya watu binafsi pamoja na majengo ya kibiashara yapatayo 17,000 yameharibiwa katika mashambulizi hayo yaliyodumu kwa siku 11.

Aidha Umoja wa Mataifa umesema majengo ya elimu 53, hospitali sita na vituo vya afya 11 vimeharibiwa tangu Mei 10. Shule nazo zimefungwa, hali ambayo inapelekea watoto wapatao 600,0000 kukosa elimu kwa sasa.

Naji Suhran, naibu wa wizara ya kazi na makazi ya Gaza amesema misikiti minee pia imeharibiwa pamoja na vituo kadhaa vya polisi huko Gaza. Ameongeza kwamba viwanda vingi vimeharibiwa.

Sarhan amesema hasara ya kifedha inayokadiriwa kutoka na mapigano hayo ni dola milioni 150. Amesema tathmini bado inaendelea.

Soma zaidi: Waisraeli na Wapalestina waanza kurudia maisha ya kawaida

Wakati huo huko, kufuatia ukaguzi wa polisi mkuu wa polisi Mahmoud Salah amesema wamekusanya karibu makombora 300  ya Israeli ambayo hayakulipuka.

Israel ilifanya mamia ya mashambulizi ya anga katika Ukanda huo wa Gaza wenye wakazi wengu, na kulenga majengo ya wakazi wa kawaida, ya kibiashara na ya serikali. Huku ikidai kwamba ikilenga ofisi za kundi la Hamas linalodhibiti Ukanda wa Gaza na ambalo lilikuwa likijibizana kwa mashambulizi na Israel.

Watu 250 waliuawa wengi wao wakiwa Wapalestina na kusababisha uharibifu mkubwa katika Ukanda wa Gaza eneo ambalo tayari lilikuwa na umasikini. Mapambano hata hivyo yalisimamishwa Ijumaa.

Gaza | Palästinenser feiern Waffenruhe zwischen Israel und der Hamas
Wapalestina wakishangilia kusitishwa kwa mashambuliziPicha: Ibraheem Abu Mustafa/Reuters

Wasuluhishi wa Misri wafanya mazungumzo kudumisha amani

Wakati huo huo katika juhudi za kudumisha utulivu, timu mbili za wasuluhishi kutoka Misri zimefika nchini Israel na maeneo ya Palestina kuendeleza mazungumzo ya kuimarisha makubaliano ya kusitisha mapigano na kurejesha utulivu utakaodumu kwa muda mrefu.

Kulingana na mwanadiplomasia wa Misri, ambayo imesimamia makubaliano hayo amesema majadiliano hayo yatahusisha utekelezaji wa hatua walizokubaliana kuhusu Gaza na Jerusalem, ambazo ni pamoja na namna ya kujizuia na shughuli zilizochochea makabiliano haya ya karibuni. Hata hivyo hakuelezea zaidi.

Mwanadiplomasia huyo hakutaka kutambulishwa alipozungumzia makubaliano hayo ya ndani.

Katika hatua nyingine, Misri imesema itapeleka malori 130 yatakayokuwa na misaada ya kiutu na vifaa vya tiba pamoja na dawa kwenye eneo la Ukanda wa Gaza.

US-Außenminister Antony Blinken
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony BlinkenPicha: Saul Loeb/Pool AFP/AP/picture alliance

Blinken kuzuru Mashariki ya Kati

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Anthony Blinken atazuru Israel na mamlaka ya Palestina kwenye eneo linalokaliwa kimabavu la Ukingo wa Magharibi.

Chanzo kilichoarifu kuhusiana na ziara hiyo kimesema Blinken atazuru maeneo hayo siku ya Jumatano na Alhamisi kama sehemu ya juhudi za Washington za kuimarisha makubaliano ya Gaza.

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa: Msaada wa kifedha unahitajika Gaza

Maafisa wa Marekani, Israeli na Palestina hata hivyo bado hawajachapisha ratiba ya ziara hiyo ya Blinken, lakini wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani ilitangaza ziara hiyo siku ya Alhamisi ikisema atazungumzia juhudi za kusaidia kuanza upya na kushirikiana kujenga mustakabali bora kwa Israel na Palestina.

Rais Biden tayari ameahidi kuisaidia Gaza kujijenga upya. Blinken pia atazuru Misri iliyosimamia makubaliano ya Gaza ya kusitisha mapigano kati ya mataifa hayo mawili pamoja na Jordan.

Vyanzo: rtre,ap