1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wataka uhakika wa usalama Aleppo

Sekione Kitojo
18 Oktoba 2016

Umoja wa mataifa umesema mpango wa Urusi wa kusitisha mapigano hautakuwa na maana kwamba misaada ya kiutu itaingia katika eneo la mashariki la mji wa Aleppo lililozingirwa kwa sababu bado hakuna uhakika wa usalama.

https://p.dw.com/p/2ROAK
Syrien Krieg - Zerstörung in Aleppo
Picha: Reuters/A. Ismail

Umoja wa mataifa umesema leo kwamba mpango wa Urusi wa kusitisha mapigano hautakuwa na maana kwamba misaada ya kiutu itaingia katika eneo la mashariki la mji wa Aleppo lililozingirwa kwa sababu Urusi, Syria na makundi mengine yanayopigana hayajatoa uhakika wa usalama kwa wafanyakazi wa kutoa misaada.

Wakati  huo  huo waziri  wa  mambo  ya  ndani  wa Ujerumani   Thomas de Maiziere  amesema  juhudi za  kupambana na  kundi  la  Dola  la  Kiislamu  nchini  Iraq  na  Syria  hazitaongeza kitisho cha  mashambulizi  nchini  Ujerumani.

Akizungumzia hali hiyo, msemaji wa Umoja wa Mataifa Jens Laerke ameitaka Serikali  ya  Syria  pia   kubadilisha  uamuzi  wake  wa wiki iliyopita  wa  kukataa  kuruhusu  misaada  kuingia  katika  eneo  la mashariki  la  mji  wa  Aleppo, ambako  umoja huo  unakadiria kwamba  raia  275,000  na  waasi  wapatao 8,000  wamekwama.

Syrien Krieg - Zerstörung in Aleppo
Mji wa Aleppo ulivyoharibiwaPicha: Reuters/A. Ismail

"Tunahitaji  kupatiwa  uhakika  kutoka  pande  zote katika  mzozo huo, sio  tu tangazo  la  upande  mmoja , kwamba hili litatendeka . Tunahitaji  kila  mtu  kutoa  uhakikisho  huo  kabla ya  sisi  kuweza kufanya  kitu  chochote  cha  maana  kwa  upande wa  kiut."

Kamati  ya  kimataifa  ya  msalaba mwekundu  imesema  bado haijawa  wazi  ni  muda  gani  utahitajika  kupata  uhakikisho  huo  wa usalama  kutoka  pande  zote, ikiwa  ni  pamoja  na  wapiganaji waasi.

Uharibifu wa  hospitali

Urusi  imesema  jana  kwamba  majeshi  ya  nchi  hiyo  na  Syria yanasitisha  mapigano  katika  mji  wa  Aleppo kwa  masaa  nane siku  ya  Alhamis  kuruhusu  raia  na  waasi  kuondoka  kutoka  katika mji  huo, na  leo  wamesitisha  mashambulizi  yote  ya  anga , siku mbili  kabla  ya  muda  uliotangazwa.

Laerke  aliuambia  mkutano   wa  kila  siku  wa   waandishi  habari mjini  Geneva  kwamba  Urusi  imeuambia  Umoja  wa  Mataifa kwamba  usitishaji  mapigano  ni  kwa  masaa  nane  katika  zaidi  ya siku  moja  kamili.

Mashambulizi  ya  Urusi  na  Syria  yameharibu  mahospitali  mengi katika  mji  huo  uliozingirwa, ambako  watu  406 waliuwawa  na 1,384 wamejeruhiwa  kati  ya  Septemba  23 na  Oktoba  8, kwa mujibu  wa   takwimu  za  Umoja  wa  Mataifa  kutokana  na  ripoti kutoka  mahospitali  mbali  mbali.

Syrien Krieg - Kämpfe in Aleppo
Mapigano katika eneo la mashariki la Aleppo Picha: Reuters/A. Ismail

Robert Mardini  mkurugenzi wa  kanda  wa  kamati  ya  kimataifa  ya msalaba  mwekundu  ICRC  kwa  ajili  ya   mashariki  ya  mbali  na kati , amesema , "makadirio  yetu  hivi  leo ni  kwamba  kuna makundi  karibu 50  ndani  ya  mashariki  mwa  Aleppo, na  sio  tu kuhusu  Urusi  na  serikali  ya  Syria," ameliambia  shirika  la  habari la  Reuters.

Vikwazo vya  kiuchumi

Pamoja  na  hayo  kansela  wa  Ujerumani Angela  Merkel  amesema haondoi  uwezekano  wa  Urusi  kuwekewa  tena  vikwazo  vya kibiashara  kutokana  na  hatua  zake  nchini  Syria.

Mke  wa  rais  wa  Syria  Asma al-Assad  wakati  huo  huo amesema  amekataa  maombi  kadhaa  ya  kukimbia  vita  pamoja na  watoto  wake , kwa  mujibu  wa  mahojiano  aliyofanya  na  kituo cha  televisheni  cha  Russia  24 yaliyorushwa  hewani  leo Jumanne.

Asma Al Assad
Mke wa rais wa Syria Asma al-AssadPicha: picture-alliance/dpa

Nae  waziri  wa   mambo  ya  ndani  wa  Ujerumani  Thomas de Maiziere  amesema  maafisa  wanatarajia  wapiganaji  wa  IS kutoka Ulaya  watajaribu  kurejea  nyumbani  wakati  kundi  hilo likikabiliwa na  kupoteza  maeneo , lakini  maafisa  wanaifanyia  kazi  hali  hiyo kupunguza  kitisho  cha  usalama.

Mwandishi:     Sekione  Kitojo / rtre  / ape / afpe

Mhariri:  Daniel Gakuba