1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wasema bado IS ni hatari Afrika Magharibi

Tatu Karema
16 Februari 2024

Umoja wa Mataifa unasema kundi linalojiita Dola la Kiislamu (IS) linaendelea kuwa tishio huku kukiwa na ukosefu wa utulivu wa kisiasa Afrika Magharibi na katika eneo la Sahel na bado lina nia ya kufanya mashambulizi.

https://p.dw.com/p/4cSv3
Filamu ya wapiganaji wa Sahel.
Baadhi ya wapiganaji wa makundi ya siasa kali katika Ukanda wa Sahel katika filamu fupi.Picha: Inside the Resistance

Kwa mujibu wa Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kukabiliana na Ugaidi, Vladimir Voronkov, amesema matokeo ya utafiti wa ofisi yake yanaonesha kwamba kundi hilo linaendelea kutishia amani na usalama wa kimataifa, hasa katika maeneo yenye migogoro, licha ya ufanisi mkubwa wa mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa katika kukabiliana na tishio hilo.

Soma zaidi: Ujerumani yachukua urais wa muungano wa kanda ya Sahel

Voronkov aliongeza kuwa kundi hilo pia limeimarisha operesheni zake katika ngome za awali za Iraq na Syria pamoja na kusini mashariki mwa Asia.

Voronkov aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa katika eneo la Afrika Magharibi na Sahel, hali imezidi kuwa mbaya na ngumu zaidi.