1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa mataifa warefusha ujumbe wa Umoja wa Afrika , Somalia.

Mohammed Abdul-Rahman21 Agosti 2007

limewataka wanachama kuchangia kwa fedha, watumishi na vifaa kufanikisha jukumu hilo.

https://p.dw.com/p/CH9J
Wanajeshi wa umoja wa Afrika nchini Somalia
Wanajeshi wa umoja wa Afrika nchini SomaliaPicha: AP

Baraza la usalama la umoja wa mataifa limerefusha ujumbe wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia, wakati likiendelea kuandaa mpango juu ya uwezekano wa kjutumwa kikosi cha kusimamia amani cha umoja wa mataifa katika taifa hilo la pembe ya Afrika,lililoharibiwa kwa vita.

Ujumbe wa umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM ulianza shughuli zake Februari mwaka huu kwa lengo la kuupa msukumo mjadala wa kitaifa nchini Somalia kwa kusaidia katika kuwalenda wanaoshiriki katika mwenendo huo pamoja na taasisi za mpito nchini Somalia.´

Baraza la usalama la umoja wa mataifa lenye wanachama 15, limezitaka nchi wanachama zichangie kwa fedha, watumishi, vifaa na huduma kwa ajili ya ujumbe huo nchini Somalia.

Zaidi ya hayo azimio la baraza hilo limemtaka katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-Moon ashauriane na halmashauri kuu ya umoja wa Afrika, juu ya msaada zaidi utakaohitajika klutoka umoja wa mataifa ili kusaidia shughuli za ujumbe huo nchini Somalia.

Aidha azimio pia limemtaka katibu mkuu huyo aendelee na mipango ya uwezekano wa kutumwa ujumbe wa kusimamia amani wa umoja wa mataifa kuchua nafasi ya ule wa umoja wa Afrika, akiombwa kutuma ujumbe wa kiufundi kutathimini hali ya mambo ilivyo haraka iwezekanavyo.

Sambamba na hayo baraza la usalama la umoja wa mataifa limeyataka mataifa wanachama yenye ndege za kijeshi au vituo vya jeshi la majini karibu na Somalia kuwa makini dhidi ya vitendo vyovyote vya kiharamia na kuzilinda meli za biashara zinazosafiri eneo la maji karibu na Somalia na hasa zinazosafirisha misaada ya kiutu inayohitajika.

Umoja wa mataifa uliidhinishwa kutumwa wanajeshi 8,000 wa umoja wa Afrika nchini Somalia baada ya majeshi ya serikali yakisaidiwa na majeshi ya Ethiopia kuwashinda wana mgambo wa muungano wa maahakama za Kiislamu waliokua wakiudhibiti mji wa Mogadishu na sehemu kubwa za kusini mwa nchi hiyo. Lakini miezi sita baadae ni wanajeshi 1,800 tu kutoka Uganda waliopelekwa Somalia, idadi ndogo mno kuliko ile inayohitajika.

Akizungumza na Redio Deutsche welle kuhusu uamuzi huo wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa kurefusha muda wa ujumbe wa Umoja wa Afrika nchini Somalia, mshauri maalum wa rais wa Somalia Abdulahi Yussuf Ahmed, Bw Abdulrazak Hussen Adem alissema « Wanajeshi wa kusimamia amani wa umoja wa Afrika wamefanya kazi nzuri na sawa sawa, sasa ni wakati umefika kwa hailo kutanuliwa na kuwa na walinzi wa aman wa umoja wa mataifa nchini Somalia «

Kwa mujibu wa umoja wa mataifa, mamia kwa maelfu ya watu wameuhama mji mku wa Somalia Mogadishu, tangu mapigano makali yalipozuka mwezi Februari. Uhasama katika nchi hiyo ambayo haikua na serikali kwa muda wa miak 16 uliibuka tena mwaka jana kwa kuzuka miripuko kadhaa mjini Mogadishu mwezi Desemba, huku serikali ya mpito inayosaidiwa na wanajeshi kutoka nchi jirani ya Ethiopia ikiyalaumu makundi ya kiislamu kwa hujuma hizo.