1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waomba msaada wa dola bilioni 2.4 kwa Yemen

Saleh Mwanamilongo
29 Mei 2020

Mkuu wa shirika la umoja wa mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura,OCHA, ameomba dola biliioni 2.4 kwa ajili ya misaada ya kiutu nchini Yemen.

https://p.dw.com/p/3cz50
Jemen Darwan Flüchtlingslager
Picha: picture-alliance/AA/M. Hamoud

Yemen inakabiliana na janga la Ugonjwa wa Covid-19, kando na janga la kibinadamu ambalo limekuwa likiikumba kutokana na vita pamoja na maradhi. Mkuu wa OCHA Marc LowCock ameeleza kuwa hali nchini humo inatia wasiwasi. 

Kwenye kikao cha umoja wa mataifa cha kuijadili Yemen, Marc LowCock ,mkuu wa shirika la OCHA,amesema kwamba mwaka uliopita shirika lake lilikusanya dola bilioni 3.2 kwa ajili ya Yemen kwa sababu wahisani zikiwemo Saudi Arebia na Umoja wa Falme za Kiarabu UAE, nchi zinazoshiriki kwenye mzozo huo, zilichangia kikamilifu.

Mwaka huu Umoja wa Mataifa unahitaji dola bilioni 3.4 ili kuhakisha kwamba operesheni za misaada ya kibinadamu zinaendelea nchini Yemen, lakini hadi Jumatano ni dola milioni 516 zilizokusanywa na Umoja wa Mataifa,sawa na asilimia 15 pekee. Saudi Arabia iliahidi dola milioni 525, na Lowcock amesema anategemea kwamba ahadi hiyo itakamilika.

Jumanne ijayo, Umoja wa Mataifa na Saudi Arabia zinatarajiwa kuitisha mkutano wa wahisani kwa njia ya vidio kwa ajili ya Yemen. Mkuu wa shirika la OCHA, Marc Lowcock amesema kwamba alijadiliana kwa simu na viongozi wa nchi za ghuba,lakini hajafahamu ni fedha kiasi gani watachangia.

Umoja wa Mataifa wasema hali nchini Yemen inatia wasiwasi zaidi
Umoja wa Mataifa wasema hali nchini Yemen inatia wasiwasi zaidiPicha: DW/Mohammed Baramadah

Majadiliano zaidi ya wahisani

Kuporomoka kwa bei ya mafuta kutokana na janga hili la Covid-19 kutasababisha kuwepo na majadiliano zaidi baina ya wahisani, alisema.

Yemen inamahitaji makubwa ya msaada alisema kwa upande wake Muhannad Hadi,mkuu wa shirika la mpago wa chakula duniani.

Henrietta Fore,mkuu wa shirika la watoto la umoja wa mataifa UNICEF alisema kwamba zaidi ya watoto ilioni 12 wanahitaji msaada wa kibinadamu na wamekumbwa na utapia mlo uliokithiri. Kabla ya janga la Corona watoto milioni mbili walikuwa hawaendi shule na kutokana na janga hili ni watoto milioni tano wa ziada ambao hawaendi shule,alisema Bi Fore.

Yemen iliingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo mwaka wa 2014 baada ya waasi wa kabila la Houthi,wanaoungwa mkono na Iran kuudhibiti mji mkuu Sanaa na maeneo mengine ya nchi hiyo, hali iliyoilaazimu Saudi Arabia, UAE na mataifa mengine ya Kisunii kuingilia kati.

Vyanzo:AFPE