Umoja wa Mataifa wahitaji dola bilioni 2.2 za msaada Ukraine | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.04.2022
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Mataifa wahitaji dola bilioni 2.2 za msaada Ukraine

Takriban watu watano wameuawa na wengine 18 kujeruhiwa katika shambulizi la roketi la Urusi mjini Vinnytsia. Huku Umoja wa Mataifa ukiongeza maradufu ombi lake la msaada wa dharura wa kibinadamu nchini Ukraine.

Ofisi ya mwendesha mashtaka wa mji wa Vinnytsia imesema watu watano waliuawa na wengine wasiopungua 18 kujeruhiwa kufuatia mashambulizi ya anga ya jeshi la Urusi.

Jumatatu, mripuko wa kombora pia ulizua moto katika kituo cha reli cha Krasne, karibu na mji wa Lviv, magharibi mwa Ukraine. Kulingana na gavana wa mkoa huo, hakukuwa na taarifa za waliouawa ama kujeruhiwa.

Mapema leo, jeshi la Urusi lilisema Ukraine ilizuia uhamishaji wa raia kutoka kiwanda cha chuma cha Azovstal mjini Mariupol, licha ya kutangaza kusitisha mapigano kwa upande mmoja. Ukraine inapinga madai hayo, ikisema Moscow haikukubaliana na ombi lake la kuhamishwa kwa wanajeshi na raia waliojeruhiwa.

Soma pia→Austin: Ukraine inaweza kuishinda Urusi

Moldova kuitisha mkutano wa kiusalama

Raia wa Moldova wakiandamana kwenye ubalozi wa Urusi

Raia wa Moldova wakiandamana kwenye ubalozi wa Urusi

Rais wa Moldova, mojawapo ya jamhuri za zamani za Sovieti, ameitisha mkutano wa baraza la usalama la nchi hiyo baada ya mfululizo wa miripuko katika eneo la Transnistria linaloungwa mkono na Urusi. Moldova ambayo inapakana na Ukraine upande wake wa mashariki, ilishuhudia miripuko kwenye wizara yake ya usalama siku ya Jumatatu na mnara wa redio leo asubuhi.

Huku hayo ya kijiri, Umoja wa Mataifa umetangaza kwamba umeongeza ombi lake la msaada wa dharura wa kibinadamu nchini Ukraine mara mbili zaidi na sasa unahitaji jumla ya dola bilioni 2.2.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya Kibinaadamu, OCHA, limesema kwenye taarifa kwamba fedha hizo zinahitajika haraka kwa mahitaji ndani ya Ukraine. Hiyo ni zaidi ya mara mbili ya kiasi kilichoombwa cha dola bilioni 1.1 mnamo Machi 1, siku chache baada ya vita kuanza.

Soma pia →Rais wa halmashauri kuu EU akutana na waziri mkuu India Narendra Modi

Wakimbizi kufikia milioni 8.3

Wakimbizi wa Ukraine wazidi milioni 5.2

Wakimbizi wa Ukraine wazidi milioni 5.2

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa idadi ya wakimbizi wa Ukraine walioikimbia nchi yao iliyovamiwa Februari 24 na jeshi la Urusi inaweza kufikia milioni 8.3 hivi sasa.

Kwa upande wake, kwa kuzingatia kuzorota kwa hali ya wakimbizi, Kamishna Mkuu wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa ameomba dola bilioni 1.8 kusaidia hatua zake na za washirika wake kwa ajili ya watu hao wanaokimbia vita.

Shirika la ushirikiano wa mahakama la Umoja wa Ulaya linasema mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, ataungana na timu ya uchunguzi ya Umoja wa Ulaya kuchunguza uwezekano wa uhalifu wa kimataifa uliofanywa nchini Ukraine. Itakuwa ni mara ya kwanza wameshiriki katika uchunguzi wa pamoja wa kimataifa.