Umoja wa Mataifa wafadhaishwa na taarifa za vitendo vya ubakaji katika jimo la Tigray | Matukio ya Afrika | DW | 22.01.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Ethiopia

Umoja wa Mataifa wafadhaishwa na taarifa za vitendo vya ubakaji katika jimo la Tigray

Umoja wa Mataifa wasema umepokea ripoti za kufadhaisha za matukio ya unyanyasaji wa kijinsia katika jimbo la Tigray liliokumbwa na mizozo nchini Ethiopia. 

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia maswala yanayohusu tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia, Pramila Patten amesema kuna taarifa kwamba unyanyasaji wa kingono unatokea katika jimbo la Tigray huku wanawake na wasichana wakiwa wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa vifaa vinavyoweza kuwasaidia kutokana na dhuluma hiyo ya ubakaji pamoja na dawa za kufubaza VVU.

Hayo ni kutokana na vizuizi vilivyowekwa ambapo imekuwa ni vigumu kwa mashirika ya kutoa misaada kuweza kuwafikia wahanga wa ubakaji. Patten amesema pia kuna taarifa kwamba baadhi ya watu wanalazimishwa kuwabaka wanawake ndani ya familia zao katika mateso yanayoambatana na vitisho.

Soma zaidi:Zaidi ya watu 80 wauwa katika shambulizi Ethiopia

Wakati huo huo wakimbizi wapya wanaofika katika kambi za wakimbizi wa ndani pia wametoa taarifa za kuwepo unyanyasaji wa kijinsia, dhidi ya wanawake na wasichana ndani ya kambi hizo.

Patten pia ameeleza wasiwasi wake juu ya zaidi ya wakimbizi 5,000 wanaoishi katika hali mbaya, wengi wao wameripotiwa kuwa wanalala katika uwanja ulio wazi bila maji au chakula. Zaidi ya Waethiopia 59,000 wameikimbia nchi yao na kuingia katika nchi jirani ya Sudan.

Wakimbizi wa Ethiopia katika kambi ya Um Raquba nchini Sudan

Wakimbizi wa Ethiopia katika kambi ya Um Raquba nchini Sudan

Bibi Patten kwenye taarifa yake ameeleza juu ya wanawake wengine wanaoripotiwa kulazimishwa na wanajeshi kushiriki ngono kwa ajili ya kupata mahitaji ya msingi. Msemaji wa ofisi ya Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia maswala unyanyasaji wa kijinsia hata hivyo hakutaja ni vikosi gani vya jeshi vinavyohusika na tuhuma hizo. Wapiganaji walioko katika jimbo hilo la Tigray ni pamoja na wale wanaotoka kwenye mkoa wa jirani wa Amhara na maeneo mengine ya Ethiopia pamoja na wanajeshi kutoka nchi jirani ya Eritrea.

Angalia:

Tazama vidio 01:41

Mzozo wa Tigray waendelea kutokota

Miito inazidi kuongezeka kwa serikali kuu ya Ethiopia juu ya uwezekano wa kuingia katika jimbo la Tigray bila masharti. Mkoa huo ulikumbwa na mapigano mwanzoni mwa Novemba mwaka uliopita kati ya vikosi vya serikali kuu ya Ethiopia na vikosi vilivyo chini ya uongozi wa Tigray.

Kwa upande wake serikali ya Ethiopia imesema misaada imeanza kuingia katika eneo la Tigray, lakini tamko hilo limepingwa na wafanyikazi wa mashirika yanayotoa misaada ambao wameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba bado zoezi linakwenda taratibu mno.

Vyanzo:AFP/AP