1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waagiza wanajeshi kuwa macho Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo

15 Desemba 2010

Kitisho cha waasi wa LRA kufanya mauaji wakati wa msimu wa sikukuu ya Krismasi kimechomoza, huku taarifa zikidhihirisha kuwa waasi hao wamekuwa wakiwaua na kuwateka nyara watu

https://p.dw.com/p/QcL7
Waasi wa kundi la LRAPicha: picture-alliance/ dpa

Umoja wa mataifa umeagiza askari 900 wa kulinda amani katika maeneo ya mashambani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kuwa macho kutokana na hofu ya mashambulio yanayoweza kufanywa katika sikukuu za Krismas na kundi la waasi wa Lord's Resistance Army, LRA

Vikosi vya Umoja wa Mataifa vitaweka kambi katika eneo ambalo waasi wa Lord's Resistance Army waliwaua watu pamoja na watoto zaidi ya 1,000 katika kipindi cha sikukuu ya Krismasi mwaka 2008 na 2009 na kuteka nyara zaidi ya watu 100.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Martin Nesirky amesema ujumbe wa umoja wa mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unasambaza zaidi mahitaji ya kibinadamu nchini humo.

Oparesheni maalumu dhidi ya waasi wa LRA imezinduliwa katika Wilaya ya Dungu iliyopo katika eneo la uwanda wa juu, Mkoani Uele. Oparesheni hiyo itaendelea mpaka katikati ya mwezi January kutokana na hofu ya mashumbulio katika kipindi cha sikukuu za krismasi.

Tangazo hilo limekuja baada ya baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka jitihada za kimataifa dhidi ya kundi la waasi wa LRA, linaloongozwa na Joseph Kony ambaye anatafutwa na mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai kutokana na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.

Kindersoldaten - Joseph Kony
Kiongozi wa LRA, Joseph KonyPicha: picture-alliance/ dpa

Kundi la LRA liliibuka kuwa waasi nchini Uganda katika miaka ya 1980 na mpaka hivi sasa linazitia hofu jamii za watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan ya Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, limeukaribisha mpango wa Umoja wa Afrika kuunga mkono jitihada za kuikabili LRA na kusaidia ukaguzi katika maeneo ya mipakani.

Maelezo ya baraza la usalama katika jitihada za kuleta amani katika jamhuri ya Afrika ya kati imezitaka nchi katika eneo hilo la Afrika ya kati kuongeza ushirikiano na kupeana taarifa kulingana na vitisho vinavyotolewa na waasi wa LRA.

Jeshi maalumu nchini Uganda hivi sasa linaongoza mpango wa kimataifa wa kumtafuta Kony ambaye anatafutwa na mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai kutokana na makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya haki za binadamu.

Mnamo mwaka 2008, wapiganaji wa LRA waliwauwa watu 865 wakiwemo wanawake na watoto kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kusini mwa Sudan, na kuteka nyara zaidi ya watu 100.

Mwaka mmoja baadaye watu 300 waliuwawa mwezi Disemba katika kipindi cha tarehe 14 na 17 Kasakzini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Serikali ya Marekani imeahidi kusaidia mpango mpya wa kumkamata Kony na kusimamisha mapigano yanayofanywa na kundi la waasi wa LRA. Lakini kwenye ripoti inayoitwa, jinamizi la krismas iliyopita. Mashirika 19 ya misaada yamesisitiza baraza la usalama kutilia mkazo suala hilo.

Ripoti imeleeza kuwa waasi wa LRA wanawashambulia raia wanaoishi mashambani mara nne kwa mwezi, Sudan ya kusini, Jamhuri ya Afrika ya kati na Jamhuri ya kidemokrasia ya kongo.

Mashirika ya misaada ya Oxfam, Christian Aid, Refugees International, World Vision na War Child UK, yamesema jamii hizo zinaisubiri sikukuu ya krismas kwa hofu.

Shirika la wakimbizi la umoja wa mataifa, mwezi Oktoba limesema waasi wa LRA tangu mwezi Disemba mwaka 2008 limewaua watu 2000. Limeteka nyara zaidi ya watu 2,600 na kuwaacha bila makazi watu 400,000 katika Jamhuri ya kidemokrasia ya kongo, Sudan ya kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Tabu za maisha na watu kuachwa bila makazi kunakofanywa na waasi wa LRA, kunaendelea kuvuka mipaka ya kimataifa na kudhoofisha uthabiti wa nchi ambazo tayari ni dhoofu, wakati ambapo Sudan ya kusini inajiandaa na mpango wa kura za maoni kwa ajili ya kujitenga mapema mwaka 2011.

Mashirika ya misaada yameikaribisha hatua ya hivi karibuni ya serikali ya Marekani na Umoja wa Afrika, lakini mashirika yameeleza kuwa watu waliotekwa nyara lazima wasaidiwe kurudishwa nyumbani kwao na vijiji lazima vilindwe.

Mashirika hayo yamelitaka baraza la usalama la umoja wa mataifa kutafuta wataalamu kwani kumekuwa na ukosefu wa mawasiliano kuhusu kundi la waasi wa LRA mahali walipo, muundo wao na motisha wanayoipata inayosababisha kufanya uasi.

Waasi wa LRA waliibuka kaskazini mwa Uganda mwishoni mwa miaka ya1980 na hawakufanya shambulio lolote tangu mwaka 2006.

Tangu mazungumzo ya amani ya Sudani ya kusini yavunjike mwaka 2008, wapiganaji wa LRA wamekuwa wakizungukia vichaka katika eneo la Afrika ya Kati na kulaumiwa mara kwa mara kuwachinja raia wasio kuwa na hatia. Umoja wa Afrika umesema Kundi la LRA linatakiwa kuitwa kundi la magaidi na sio kundi la waasi.

Mwandishi: Fatuma Matulanga/AFP

Mhariri:Josephat Charo