1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa: Msaada wa kifedha unahitajika Gaza

20 Mei 2021

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRA, limetoa rai ya kupatiwa dola milioni 38 kwa ajili ya msaada wa dharura unaohitajika kwenye Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/3tgNY
Palästina-Israel Konflikt Gaza Streifen
Wengi ya Wapalestina wamepoteza au kuyakimbia makaaziPicha: Ali Jadallah/AA/Getty Images

Shirika hilo limesema msaada huo unahitajika haraka kugharamia mahitaji ya dharura huko Gaza ikiwemo chakula, maji, huduma za afya na msaada wa kisaikolojia kwa wahanga wa machafuko yanaoendelea kati ya Israel na kundi la Hamas linalotawala eneo hilo.

Kadhalika kiwango hicho cha fedha kitatumika pia kusambaza mahitaji ya dharura kwenye Ukingo wa Magharibi ikiwemo eneo la Jerusalem Mashariki.

UNRA imesema tayari wafanyakazi wake wanaendelea kusaidia idadi kubwa ya wapalestina walio na wasio wakimbizi ikiwemo mamia kwa maelfu ya watu wanaotafuta maeneo salama ya kujihifadhi kwenye shule na makaazi ya dharura yaliyotengwa na shirika hilo.

Palästina-Israel Konflikt Gaza Streifen
Maelfu ya Wapalestina wanakwenda kwenye vituo vya dharura kupata malazi na chakula Picha: Ali Jadallah/AA/Getty Images

Wito wa shirika la UNRA unatolewa wakati Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limesema leo kuwa litafanya kikao cha dharura wiki inayokuja kujadili "hali inayotia wasiwasi ya haki za binadamu" kwenye maeneo ya Palestina ya Ukingo wa Magharibi, Ukanda wa Gaza na Jerusalem Mashariki.

Kikao hicho cha Mei 27 kitafanyika kutokana na ombi lililotolewa na Pakistan na  kuungwa mkono na zaidi ya nchini wanachama 60.

Kikao hiccho kitatoa nafasi ya mjadala wa siku nzima kuhusu machafuko yanyoendelea sasa kati ya Israel na kundi la Hamas, mzozo ambao umedumu kwa miongo kadhaa.

Juhudi za kusitisha mapigano bado zinajikongoja 

Wakati hayo yakiarifiwa juhudi za kimataifa za kutuliza mapigano bado zinaendelea.

Mapema leo Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alisema mazungumzo na kundi la Hamas ni muhimu ili kufanikisha usitishaji mapigano kwenye mzozo huo wa Mashariki ya Kati.

Palästina UN Nothilfe
Picha: Mohammed Abed/AFP/Getty Images

Kwenye mahojiano na waandishi habari Merkel amependekeza kuwepo mashaurino yasiyo ya moja kwa moja na kundi la Hamas kupitia mataifa ya kiarabu kama Misri yatakayosaidia kumaliza mvutano wa sasa na kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro kati ya Israel na Palestina.

Kwengineko juhudi za kutafuta suluhu ya mzozo huo zimeingia ganzi baada ya Marekani kulipinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotoa wito wa kusitishwa kwa mapigano kati ya Israeli na wapiganaji wa Hamas.

Marekani imesema azimio hilo lililoandaliwa na Ufaransa linaweza kutatiza hatua zinazochukuliwa na utawala wa rais Joe Biden wa kumaliza uhasama kati ya Israel na Palestina.

China kwa upande wake imesema inafanya kazi kubwa ya upatanishi kwenye mapigano yanayoendelea na kwamba mjumbe wake maalamu kwa Mashariki ya Kati Zhai Jun amezungumza na wawakilishi wa Israel, Urusi, Marekani na Umoja wa Ulaya.

Zhai amehimiza kusitishwa kwa mapigano na kwamba China inaunga mkono pendekezo la kuwepo mataifa mawili kama suluhisho na mzozo huo wa Mashariki ya Kati.