1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji Hongo waitia kishindo China

Iddi Ssessanga
9 Juni 2019

Makundi ya demokrasia yanatizamia maandamano makubwa zaidi tangu 2003, kupinga muswada wa sheria ya kuwapeleka watuhumiwa China. Shinikizo la kimataifa pia linaongezeka, kutoka hasa Marekani na Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/3K6aK
Hong Kong - Demonstration gegen das Zulassen der Auslieferungen nach China
Picha: picture-alliance/AP PHoto/V. Yu

Hong Kong imetumbukia katika mgogoro mpya wa kisiasa baada ya mamia kwa maelfu ya watu kushiriki maandamano kupinga sheria inayopendekezwa, ambayo itaruhusu watuhumiwa kupelekwa China bara kukabiliwa na mashtaka.

Waandaji wa maandamano hayo wamesema makadirio yao ya awali yanaonyesha zaidi ya washiriki nusu milioni. Ushiriki wa Jumapili umezidisha shinikizo kwa mtendaji mkuu wa Hong Kong Carrie Lam na maafisa wanaomuunga mkono mjini Beijing.

Maandamano hayo yamehitimisha wiki kadhaa za ongezeko la hasira miongoni mwa jumuiya za wafanyabiashara, wanadiplomasia na wanasheria, ambao wanahofia kuondolewa kwa uhuru wa kisheria wa Hong Kong, na ugumu wa kuhakikisha ulinzi wa msingi wa kimahakama katika China bara.

Koloni hilo la zamani la Uingereza, lilikabidhiwa tena kwa utawala wa China mwaka 1997, kwa uhakikisho wa kulinda mamlaka yake ya ndani na baadhi ya uhuru, ikiwemo mfumo tofauti wa kisheria, ambao wanadiplomasia wengi na viongozi wengi wa biashara wanaamini ndiyo kitu pekee kilichosalia kuwa imara katika mji huo.