1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu waadhimisha miaka 20 tangu mashambulio ya 9/11

Zainab Aziz Mhariri: Amina Mjahid
11 Septemba 2021

Rais wa Marekani Joe Biden atayatembelea maeneo matatu yaliyoshambuliwa mnamo 9/11- mwaka 2001 huku viongozi wa ulimwengu wakiendelea kutuma ujumbe kwa kiongozi huyo na watu wa Marekani.

https://p.dw.com/p/40CFd
USA | Terroranschlag am 11. September 2001
Picha: Jose Jimenez/Primera Hora/Getty Images

Rais wa Marekani Joe Biden amesema umoja wa kitaifa ndiyo nguvu kubwa kabisa ya Marekani, katika ujumbe wake wa kumbukumbu ya miaka 20, tangu mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11. Biden amesema pamoja na hisia kali za umoja wa kitaifa, baada ya tarehe 11 Septemba 2001, Marekani imeshuhudia pia ushujaa kila mahali.

Rais wa Marekani Joe Biden
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Kevin Lamarque/REUTERS

Msemaji wa ikulu ya Marekani, Jen Psaki, amesema Rais Biden na mkewe, watakwenda kutoa heshima zao, kwa wahanga wa mashambulizi hayo, katika maeneo matatu yaliyoshambuliwa ambako ni  New York City, Penn-sylvania, na Pentagon.

Mashambulio hayo ya kigaidi ya Septemba 11, mnamo mwaka 2001 yalisababisha vifo vya watu 2,977.

Clifford Chanin makamu mtendaji mkuu wa ukumbi wa Makumbusho ya Kitaifa ya Septemba 11 uliojengwa katika eneo la shambulio kwenye Kituo cha Biashara Ulimwenguni, (World Trade Center) amesema maadhimisho hayo yatatafakari hisia nyingi kwa nchi hiyo kwa kuzingatia wapi wamarekani walipo, wapi walipokuwa na wanakoelekea.

Jumba la makumbusho ya mashambulizi ya 9/11 mjini New York
Jumba la makumbusho ya mashambulizi ya 9/11 mjini New YorkPicha: Spencer Platt/Getty Images

Katika Jiji la New York, maadhimisho ya kumbukumbu za Septemba 11 yataanza kwa watu kunyamaa kimya hapo saa mbili na dakika 46 asubuhi kwa saa za Marekani wakati ambapo ndege ya kwanza ilivamia moja wapo ya minara pacha ya Kituo cha Biashara Ulimwenguni. Baada ya hapo wanafamilia watasoma majina ya watu 2,977 waliokufa kwenye mashambulio hayo. Hafla hiyo ya kila mwaka huchukua takriban masaa manne. Baada ya hapo rais wa Marekani Joe Biden atakwenda Shanksville, Pennsylvania, ambako ndege ya United Flight 93 ilianguka kwenye uwanja baada ya abiria kuwadhibiti watekaji nyara, hatua iliyowezesha kuzuia shabaha nyingine kushambuliwa.

Rais huyo wa Marekani atamaliza siku katika eneo la Washington DC kwa kuitembelea Pentagon, ambayo pia ilishambuliwa mnamo 9/11.

Marekani yaadhimisha miakam 20 tangu mashambulio ya 9/11 ya mwaka 2001
Marekani yaadhimisha miakam 20 tangu mashambulio ya 9/11 ya mwaka 2001Picha: picture alliance / zz/Larry Le Vine/STAR MAX/IPx

Mashambulizi hayo ya kigaidi kwa kutumia ndege za abiria, ndiyo pekee yaliyowahi kufanywa na maadui wa kigeni ndani ya ardhi ya Marekani, katika historia ya taifa hilo lenye nguvu kubwa za kijeshi ulimwenguni, na iliyatumia kama sababu ya kuvamia Afghanistan na Iraq.

Kumbukumbu ya 9/11 ya mwaka huu inafanyika ikiwa ni  muda mfupi tangu Marekani kumaliza uwepo wa majeshi yake nchini Afghanistan, ambayo yalikuweko miaka 20 iliyopita kwa ajilim ya kupambana na magaidi wa kundin la al Qaeda, ambalo lilifanya mashambulio ya 9/11 nchini Marekani mnamo mwaka 2001.

Wanajeshi wa Marekani walipokuwa nchini Afghanistan
Wanajeshi wa Marekani walipokuwa nchini AfghanistanPicha: John Moore/Getty Images

Hata hivyo hatua ya Biden ya kuwaondoa wanajeshi wa Marekani mnamo mwezi Agosti, kutoka nchini Afghanistan ikiwa ni miezi kadhaa baada ya tarehe ya mwisho iliyowekwa na mtangulizi wake, Donald Trump, na nchi hiyo kuingia kwa kasi mikononi mwa Taliban kumesababisha lawama na ukosoaji mkubwa kutoka kwa wanachama wa vyama vyote vya kisiasa nchini Marekani.

Vyanzo:/RTRE/https://p.dw.com/p/40Bkk