1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Ulaya yaungana dhidi ya mapinduzi ya kijeshi Myanmar

Mohammed Khelef
1 Februari 2021

Serikali za mataifa ya Umoja wa Ulaya zimeungana na jumuiya ya kimataifa kulaani mapinduzi ya kijeshi nchini Myanmar na kutowa wito wa kuachiliwa mara viongozi wa kiraia wanaoshikiliwa na jeshi baada ya mapinduzi hayo.

https://p.dw.com/p/3oftY
Myanmar Militärputsch | Militär in Naypyitaw
Picha: REUTERS

Kutoka nchi ndogo kabisa ya Umoja wa Ulaya, Luxembourg, hadi mataifa makubwa ya Ujerumani na Ufaransa, viongozi wakuu wa serikali na mawaziri wa mambo ya kigeni wanatoa kauli moja inayofanana dhidi ya mapinduzi hayo, ingawa kwa maneno ya tahadhari na yanayoepuka kuelezea kwa undani. 

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, na Rais wa Kamisheni ya Umoja huo, Ursula von der Leyen, wametowa taarifa zinazolaani mapinduzi hayo. 

Huku Borrell akisema lazima demokrasia ishinde, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Denmark, Jeppe Kofod, ameandika kwenye Twitter kwamba: "Jeshi linalodhibitiwa  na utawala wa kiraia ndio msingi mkuu wa demokrasia."

Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez, ametowa wito wa kuachiliwa mara moja kwa waliotiwa nguvuni na jeshi na kurejeshwa tena utawala wa kidemokrasia. 

Kauli kama hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian, ambaye kutiwa nguvuni kwa viongozi wa kiraia na kuhamishia madaraka jeshini hakukubaliki na ni kitisho kwa utaratibu wa demokrasia ulioanza miaka kumi iliyopita.

Suu Kyi hatajwi kwa jina

Myanma State Counsellor Aung San Suu Kyi
Kiongozi wa kiraia wa Myanmar, Aung San Suu Kyi.Picha: Athit Perawongmetha/REUTERS

Hata hivyo, ni serikali chache za Ulaya zilizomtaja moja kwa moja kwa jina Aung San Suu Kyi, ambaye ni miongoni mwa waliotiwa nguvuni. Kutomtaja kwa jina kunaashiria msimamo wa Umoja huo juu ya kile unachosema ni kushindwa kiongozi huyo kukemea kampeni ya kijeshi dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini mwake.

Licha ya kuwahi kutunukiwa Tuzo ya Haki za Binaadamu ya Bunge la Ulaya mnamo mwaka 1990, Bi Aung San Suu Kyi amezuiwa kuhudhuria matukio mengine yoyote yanayohusiana na tuzo hiyo tangu Septemba mwaka jana.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Sophie Wilmes, amesema sasa serikali za mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya zitajadiliana hatua zinazofuatia baada ya matamko hayo, ingawa hakuna waziri hata mmoja aliyekuwa tayari kusema undani wa hatua hizo.

Umoja wa Ulaya unashikilia nafasi ya tatu miongoni mwa washirika wa kibiashara wa Myanmar duniani na umeipa nchi hiyo ya Asia Kusini kipaumbele maalum, ambacho kinaweza kuondolewa licha ya hatua hiyo kuchukuwa muda mrefu kutekelezeka.

Mwaka 2018, Umoja wa Ulaya uliwawekea vikwazo majenerali wa kijeshi wa Myanmar kutokana na mauaji ya Waislamu wa jamii ya Rohingya. Umoja huo pia bado unaendeleza marufuku yake ya silaha dhidi ya taifa hilo.