1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yatakiwa kunusuru maisha

23 Aprili 2015

Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya wanaokutana kwa Mkutano wa Kilele wa dharura mjini Brussels Alhamisi (23.04.2015) wanatakiwa wachukue hatua za haraka ili kukoa maisha ya wakimbizi kwenye bahari ya Mediterenia

https://p.dw.com/p/1FDPG
Boti iliosheheni wakimbizi wanaokimbilia Ulaya.
Boti iliosheheni wakimbizi wanaokimbilia Ulaya.Picha: Marco Di Lauro/Getty Images

Kwenye kikao chao viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya pia watautathmini mpango wenye vipengele 10 juu ya kukabiliana na mgogoro wa wakimbizi baada ya maalfu ya wakimbizi kuokolewa kwenye bahari kati ya Italia na Libya katika kipindi kifupi cha wiki moja.

Rais wa Umoja wa Ulaya Donald Tusk amewataka viongozi wa nchi wanachama 28 wa umoja huo kukubaliana juu ya hatua zitakazotekelezwa kwa vitendo ikiwa ni pamoja na kuimarisha shuguli za kuwatafuta na kuwaokowa wahamiaji, kupambana watu wanaojishughulisha na kusafirisha binaadamu kwa magendo na kuwaelimisha wahanga wasikubali kuhatarisha maisha yao wakati huo huo wakiimarisha mshikamano baina ya nchi hizo wanachama katika kuushughulikia mzozo huo.

Maafisa wa Umoja wa Ulaya wamesema viongozi wa umoja huo watajitolea kuongeza maradufu juhudi za ulinzi wa mipaka katika bahari ya Mediterenia lakini operesheni hizo zitasanifiwa kwa ajili ya kufuatilia nyendo za wahamiaji na si lazima ziwe kwa ajili ya kunusuru maisha.

Mradi wa majaribio

Afisa mwandamizi wa Umoja wa Ulaya amesema viongozi hao pia wanatarajiwa kuidhinisha mradi wa majaribio wa kuwapatia makaazi mapya takriban wakimbizi 5,000.

Wakimbizi walionusurika wakiwasili Italia. (20.04.2015)
Wakimbizi walionusurika wakiwasili Italia. (20.04.2015)Picha: Reuters

Mpango huo utawahusisha nusu ya wakimbizi waliowasili wiki iliopita na sehemu ndogo ya mamia na maelfu wengine ambao yumkini wakawasili mwaka huu.

Kipengele muhimu cha mpango huo wa utekelezaji ni kupambana na watu wanaowasafirisha binaadamu kwa magendo wanaoendesha harakati zao nje ya pwani ya Libya na kuziangamiza mashua zao ili kuwazuwiya watu wasijipenyeze Ulaya.

Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binaadamu Amnesty International lenye makao yake makuu mjini London Uingereza na Shirika la Madaktari Wasiokuwa na Mipaka yanataka juhudi za kimataifa zianzishwe kusaidia maelfu wanaokimbia mizozo na umaskini kutoka katika nchi kama vile Syria,Eritrea na Somalia.

Ongezeko la vifo

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR wakimbizi na wahamiaji 219,000 walivuka bajari ya Mediterenia mwaka huu na sio chini ya 3,500 wamepoteza maisha yao wakati wakijaribu kuvuka bahari hiyo.Yumkini wakimbizi 1,000 tayari wamekufa mwezi huu pekee.

Mashua zinazotumika kuvusha wakimbizi bahari ya Mediterenia.
Mashua zinazotumika kuvusha wakimbizi bahari ya Mediterenia.Picha: imago/Anan Sesa

Watu wanalumu ongezeko la vifo hivyo kutokana na kuondolewa kwa operesheni kubwa ya uokozi ya Italia iliokuwa ikifanya kazi hapo mwaka 2013- 2014 ya Mare Nostrum ambayo ilikuwa ikifanya kazi karibu na mwambao wa Libya njia kubwa kabisa inayotumiwa na wahamiaji kukimbilia Ulaya.

Operesheni ndogo ya Umoja wa Ulaya iliopewa jina la Triton imechukuwa nafasi ya operesheni hiyo ya Italia lakini haina mamlaka ya shughuli za uokozi juu ya kwamba imekuwa ikijibu miito ya dharura kwa mujibu wa wajibu wa kimataifa na imenusuru maisha ya maelfu ya watu tokea kuzinduliwa kwake mwishoni mwa mwaka jana.

Hivi sasa mataifa matano kati ya mataifa wanachama 28 ya Umoja wa Ulaya yaani Italia,Ugiriki, Malta Ujerumani na Sweden zinapokea zaidi ya asilimia sabini ya wakimbizi wanaomiminika Ulaya.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP

Mhariri : Yusuf Saumu