1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU: Yataka ushirikiano zaidi wa kibiashara na Afrika

Amina Mjahid
27 Februari 2020

Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amefanya mazungumzo na viongozi wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, sambamba na juhudi za mkakati mpya wa Ulaya kuhusu Afrika utakaozinduliwa mwezi ujao.

https://p.dw.com/p/3YXLy
Äthiopien Ursula von der Leyen  Addis Ababa
Picha: Reuters/T. Negeri

Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen amesema Ulaya na Afrika ni washirika asilia na kusisitiza kwamba wanapaswa kushirikiana kibiashara na kupambana dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi. Katika mkutano huo, Ulaya inajaribu kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi na bara la Afrika ikilenga kuipiku China iliyowekeza kwa wingi katika bara hilo.

Lakini kulingana na Mikaela Gavas, Mkuu wa masuala ya sera katika taasisi ya maendeleo ya dunia, suala la haki za binaadamu linabakia kuwa kizingiti kikuu katika kuimarisha zaidi ushirikiano wa mabara hayo mawili.

Von der Leyen pia ameuahidi Umoja wa Afrika kuunga mkono juhudi za kumaliza ghasia barani humo ikiwa ni pamoja na Libya, akiongeza kuwa ushirikiano kati ya Ulaya na Afrika ni wenye umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya bara hilo.

"Afrika ni eneo linalokuwa zaidi kiuchumi duniani, na mataifa yenu na jamii ya kimataifa yanazidi kuungana. Kuna mambo mengi tunayopaswa kuyajadili ili tuwe na lengo moja kwaajili ya siku za usoni. Kadri Afrika inavyoimarika na sisi pia tutazidi kuimarika," alisema Von der Leyen.

Rais huyo wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya kwa sasa yuko katika mchakato wa kuzindua mkakati mpya wa Ulaya kuhusu Afrika unaotarajiwa kufanyika mapema mwezi ujao.

Mahamat asema katika baadhi ya masuala, Afrika na Ulaya wana mtazamo tofauti.

Äthiopien Addis Abeba Moussa Faki
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Moussa Faki MahamatPicha: picture-alliance/AA/M. W. Hailu

Pamoja na hayo mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amesema kuna tofauti ya namna bara la Afrika linavyoshughulikia masuala fulani ikilinganishwa na Ulaya, huku akiyaorodhesha masuala hayo kama, Masuala ya Jinai ya Kimataifa, maamuzi ya  ya kijinsia, adhabu ya kifo pamoja na masuala mengine.

Faki akizitaja tofauti hizo kama za kawaida, amesema zinaweza kukabiliwa tu kwa kuzitambua na kuzikubali.

Kwa upande wake Von der Leyen amesema anaamini Umoja huo unaweza kushughulikia tofauti zilizotajwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat

Nchi nyingi za kiafrika zimepiga marufuku masuala ya ushoga na kuufanya kuwa kosa la jinai.

Mataifa mengi ya Afrika pia yanapinga juhudi za kuwashitaki viongozi wa kiafrika katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC iliyoko the Hague Uholanzi. Mwaka 2017 Burundi ilikuwa nchi ya kwanza kujiondoa katika suala hilo.

Chanzo: AFP/dpa