1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yataka kusuluhisha mzozo Mashariki ya Kati

Lilian Mtono
14 Februari 2020

Umoja wa Ulaya umeendelea kuukosoa vikali mpango wa rais wa Marekani Donald Trump kuelekea Mashariki ya Kati ambao pia unapingwa na Palestina. Umoja huo sasa unataka kusuluhisha mzozo huo. Je, itawezekana?

https://p.dw.com/p/3Xm0S
Josep Borrell in Berlin PK
Picha: picture-alliance/dpa/A. Hosbas

Huku akiukosoa mpango wa amani wa Mashariki ya Kati wa Rais Donald Trump wa Marekani, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, amesema kunahitajika mkakati mwengine wa kumaliza mzozo kati ya Israel na Palestina.

Mkuu huyo wa sera za kigeni wa Ulaya amesema ana matumaini kwamba pande zote zitakubali Umoja wa Ulaya kuwa msuluhishi na kwamba Umoja huo unahitaji kuunda mkakati wake katika kusaidia mpango wa amani kati ya Israel na Palestina.

"Ningependa kuzungumza na mawaziri wa mambo ya kigeni wa Ulaya kuhusu kile wanachodhani Ulaya inacho na mkakati gani tunaoweza kuufanya ili kuendeleza mchakato wa amani kati ya Israel na Palestina", Borrell alisema kwenye mahojiano na gazeti la Ujerumani la Die Welt yaliyochapishwa Ijumaa (14 Februari).

Kwa mujibu wa Borrell, Umoja wa Ulaya uko mbali sana na mpango wa Marekani wa amani ya Mashariki ya Kati, na kwa pamoja, Israel na Palestina, wanatakiwa kuikubali Ulaya kuwa msuluhishi. "Inawezekana ikwa ni ngumu, lakini kila kitu kinawezekana", Borrell alisema.

Westjordanland | Israelische Siedlung Har Homa
Makazi ya Walowezi, ambayo Wapalestina wanataka Waisrael wapatao 700,000 wayaachiePicha: picture-alliance/newscom/D. Hill

Wasiwasi kuhusu uvamizi

Borrell pia alirejea upinzani wake dhidi ya mpango wa Trump , ambao utawapa Waisrael udhibiti wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi yaliyoko kwenye eneo Ukingo wa Magharibi na Mto Jordan na mwito kuhusu taifa la Palestina.

Mkuu huyo wa sera za kigeni amesema alikuwa na wasiwasi mkubwa "hususan kuhusu uwezekano wa Israel kuunyakua Mto Jordan na maeneo mengine ya Ukingo wa Magharibi kwa kuzingatia mpango huo."

Alisema hatua hiyo itakuwa ni "kinyume na sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza la Usalama la Mmoja wa Mataifa", akiongeza kwamba haitoshi kwa mpango huo kukubaliwa, kwa taifa moja kuamua kuyadhibiti maeneo mapya.

Borrell alirejea kusema tena kwamba Umoja wa Ulaya unapendelea suluhu ya mataifa mawili na mgawanyo sawa wa ardhi kati ya Israel na Palestina "kwa kuzingatia mtizamo wa Umoja wa Ulaya, lengo ni kuwa na mataifa ya Israel na Palestina yaliyo huru, ya kidemokrasia, na pande zote kuheshimiana."

21.11.2019 - Matangazo ya Asubuhi

Trump aliyasifu mapendekezo aliyoyatoa akiyataja kama "Makubaliano ya Karne," lakini kwa kiasi kikubwa yalipingwa takribani kote duniani, ikiwemo barani Ulaya. Viongozi wa Wapalestina waliyakataa mapendekezo hayo ya Marekani, tangu kabla ya kuzinduliwa na hata baada ya kutangazwa rasmi.

Wapalestina wanataka taifa huru, wakishinikiza maeneo yote yaliyochukuliwa wakati wa vita vya siku sita vya mwaka 1967, ikiwa ni pamoja na eneo la Mashariki mwa Jerusalem na Ukingo wa Magharibi. Lakini pia wanataka walowezi 700,000 wa Israel kuondoka kwenye maeneo hayo.