1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya imepokea majibu ya Iran kuhusu mkataba wa nyuklia

Grace Kabogo
16 Agosti 2022

Umoja wa Ulaya umesema umepokea majibu kutoka Iran kuhusu rasimu ya mwisho ya makubaliano ya kuufufua mkataba wa nyuklia wa Iran uliosainiwa mwaka 2015.

https://p.dw.com/p/4Fai4
Atomanlage im Iran
Picha: Alfred Yaghobzadeh/SalamPix/abaca/picture alliance

Msemaji wa mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amesema Jumanne kuwa Jumatatu jioni umoja huo ulipokea majibu yaliyokuwa katika maandishi kutoka Iran na kwamba wanayatathmini kwa sasa pamoja na kushauriana na washirika wengine wanaohusika na makubaliano hayo ikiwemo Marekani. 

Kwa upande wake Iran imesema majibu hayo ni kile ilichokieleza kuwa ni mpango wa mwisho wa kuufufua mkataba wa nyuklia uliofikiwa kati ya nchi hiyo na mataifa yenye nguvu duniani.

Harakati za kufikia makubaliano

Katika harakati za kidiplomasia, wawakilishi wa Marekani na Iran pamoja na nchi nyingine wamekuwa wakijaribu kufikia makubaliano yanayoweza kuchangia kuondolewa kwa vikwazo vya Marekani na kuendelea na vikwazo vya awali vilivyoko kwenye mkataba wa 2015 unaojulikana kwa kifupi kama JCPOA kwa ajili ya kuizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia.

Hata hivyo, mwaka 2018, Marekani chini ya utawala wa Donald Trump ilijiondoa katika mkataba huo. Jana Marekani ilisema kuwa inamuarifu Borrell kuhusu majibu yake yaliyoko katika maandishi ambayo iliyatuma Agosti 8.

Iran Teheran | Borrell Hoher Vertreter der EU und Außenminister Abdolahian
Maafisa wa ngazi ya juu wa Iran na wa Umoja wa UlayaPicha: ATTA KENARE/AFP

Ijumaa iliyopita, shirika la habari la Iran IRNA, liliripoti kuwa nchi hiyo inaweza kuikubali rasimu ya mwisho iliyopendekezwa na Umoja wa Ulaya ya kuyaokoa makubaliano hayo. Kwa mujibu wa IRNA, mwanadiplomasia wa Iran ambaye hakutaka kutajwa jina amesema mapendekezo ya Umoja wa Ulaya yanakubalika mradi tu yaihakikishie Iran juu ya masuala kadhaa yanayohusiana na vikwazo na ulinzi pamoja na masuala ambayo bado hayajatatuliwa na Shirika la Kimataifa la kudhibiti matumizi ya Nishati ya Nyuklia, IAEA.

Vikwazo viondolewe kwa vitendo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian amesema Jumanne kwamba baada ya muda mrefu wa majadiliano, kilicho muhimu kwao ni kuthibitisha kwamba vikwazo vinaondolewa kwa vitendo na Marekani kuyachukulia kwa uhalisia majibu ya Iran. ''Iwapo Wamarekani wataonesha kubadilika kiuhalisia, tutayafikia makubaliano hayo katika siku zijazo. Lakini kama Marekani haitofanya hivyo, basi hakuna kitakachofanyika,'' alifafanua Amir-Abdollahian.

Aidha, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Ned Price amesema ni juu ya Iran kufikia makubaliano ya mwisho, akikanusha madai kwamba wamejitenga na mazungumzo hayo. Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Iran na Urusi, pamoja na Marekani kwa njia isiyo ya moja kwa moja, walianza tena mazungumzo kuhusu makubaliano ya nyuklia mwanzoni mwa mwezi Agosti, baada ya kusimama kwa miezi kadhaa. Mazungumzo hayo yanayoratibiwa na Umoja wa Ulaya kuhusu kuufufua mkataba wa nyuklia wa Iran, yalianza mwezi Aprili mwaka 2021, kabla ya kusimama mwezi Machi mwaka 2022.

(DPA, AP, AFP)