1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yaipa Ugiriki miaka miwili zaidi

13 Novemba 2012

Wakopeshaji wa kimataifa wa Ugiriki wamekubaliana kuipa nchi hiyo muda wa miaka miwili zaidi ili kuhakikisha inabana matumizi na kufikia malengo ya bajeti yake.

https://p.dw.com/p/16heJ
Waziri Mkuu wa Ugiriki, Antonis Samaras (Kulia) na Rais wa baraza la Ulaya Herman Van Rompuy
Waziri Mkuu wa Ugiriki, Antonis Samaras (Kulia) na Rais wa baraza la Ulaya Herman Van RompuyPicha: picture-alliance/dpa

Hata hivyo, mataifa yanayotumia sarafu ya Euro na Shirika la Fedha la Kimataifa yamechelewesha uamuzi wa kuipatia nchi hiyo awamu nyingine ya msaada hadi wiki ijayo. Katika mkutano uliofanyika jana mjini Brussels, mawaziri wa fedha wa mataifa yanayotumia sarafu ya Euro, kwa mara nyingine wameahirisha uamuzi wa kuipatia Ugiriki msaada wa kiasi Euro bilioni 31 hadi wiki ijayo. Katika taarifa yao ya pamoja, mawaziri hao wamesema Ulaya inatambua juhudi kubwa ambazo tayari zimefanywa na Ugiriki, lakini nchi hiyo inapaswa kubana matumizi zaidi kwa mwaka mwingine ili kuruhusu uchumi wa nchi hiyo kurudi katika njia ya maendeleo endelevu.

Ugiriki yatakiwa kumaliza deni la Euro bilioni 20.7

Awali Ugiriki ilipaswa kumaliza mzigo wake mkubwa wa madeni mwaka 2014 na kwamba ilitakiwa kupunguza matumizi yake kwa kiasi cha Euro bilioni 11.5 kwa mwaka 2013 na 2014 ili kufaulu kupatiwa awamu nyingine ya msaada wa uokozi, lakini kuliko ilivyotarajiwa sasa inahitaji kupunguza matumizi kwa kiasi cha Euro bilioni 20.7. Mwenyekiti wa mawaziri wa fedha wa kundi la mataifa yanayotumia sarafu ya Euro, Jean-Claude Juncker amesema hatua za Ugiriki kubana matumizi ambazo zimeungwa mkono na wakopeshaji wa kimataifa wanaojulikana kama Troika, zitakuwa ni mageuzi sahihi.

Mawaziri wa Fedha wa EU
Mawaziri wa Fedha wa EUPicha: GEORGES GOBET/AFP/Getty Images

Juncker amesema mageuzi hayo yanayolenga kuufufua uchumi wa Ugiriki yatahusika pia katika kupunguza mzigo wake wa madeni kwa asilimia 120 ya pato lake la taifa ifikapo mwaka 2022 badala ya 2020. Amesema mkutano mwingine wa kundi la mataifa yanayotumia sarafu ya Euro utafanyika tarehe 20 ya mwezi huu wa Novemba, huku maafisa wakisema huenda yakahitajika majadiliano zaidi kuhusu kuutekeleza mpango huo mpya. Ugiriki imeidhinisha bajeti ya hatua kali za kubana matumizi kwa mwaka 2013,ambayo ilitegemewa itafikia masharti ya kupatiwa awamu ya pili ya mkopo wa Euro bilioni 31.5 za uokozi. Hata hivyo mawaziri hao wa fedha wanatarajia Ugiriki kweli itatekeleza hatua ilizojiwekea, huku baadhi wakisema ni lazima mataifa yao kuidhinisha fedha hizo.

Lagarde msisitizo zaidi unahitajika

Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa, Christine Lagarde, amesema kazi zaidi inahitajika ili kuhakikisha wanatilia mkazo zaidi hatua kali za kubana matumizi. Aidha, ripoti kuhusu hali ya kiuchumi ya Ugiriki iliyotolewa na wakopeshaji hao wa kimataifa, imeipongeza Ugiriki kutokana na juhudi zake za kutekeleza hatua za kubana matumizi. Hata hivyo ripoti hiyo imeeleza kuwa miaka miwili iliyopewa Ugiriki kufikia malengo yake ya kupunguza madeni itaacha pengo la Euro bilioni 32.6 zitakazopaswa kujazwa ifikapo mwaka 2016. Majadiliano juu ya jinsi ya kuziba pengo hilo, yatakuwa ni ajenda kuu katika mkutano ujao wa mawaziri wa fedha.

Mkuu wa IMF, Christine Lagarde
Mkuu wa IMF, Christine LagardePicha: dapd

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,DPAE
Mhariri: Daniel Gakuba