1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yatangaza vikwazo vipya dhidi ya Urusi

Zainab Aziz
16 Desemba 2022

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamemaliza mkutano wao wa kilele uliofanyika mjini Brussels kwa kutangaza hatua za kuiwekea Urusi vikwazo vipya na juu ya kutolewa fedha za ufadhili kwa Ukraine zipatazo euro bilioni 18.

https://p.dw.com/p/4L2EU
Belgien, Brüssel | EU Gipfel
Picha: Olivier Matthys/AP/picture alliance

Viongozi hao wa nchi za Umoja wa Ulaya wamemaliza mkutano wao wa mwisho katika mwaka huu wa 2022 kwa kufikia makubaliano ya kuweka awamu ya tisa ya vikwazo dhidi ya Urusi. Vikwazo hivyo vinatarajiwa kuwekwa wazi Ijumaa. Viongozi wa Umoja wa Ulaya pia walijadili njia za kuendelea kuisaidia Ukraine kukabiliana na msimu wa baridi kali ambapo wamekubaliana kuifadhili Ukraine kiasi cha Euro bilioni 18 katika mwaka ujao. Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel ameipongeza hatua ya kufikia makubaliano juu ya awamu ya tisa ya vikwazo dhidi ya Urusi.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel
Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel Picha: Nicolas Economou/NurPhoto/picture alliance

Hata hivyo mazungumzo ya viongozi hao wa Umoja wa Ulaya yalizongwa na mitazamo tofauti ya nchi wanachama pamoja na mvutano na Marekani uliosababishwa na ruzuku kwa ajili ya kampuni za nchi hiyo. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema Umoja wa Ulaya utalazimika kuchukua hatua haraka ili kukabiliana na kitisho kwa kampuni zake kutokana na mpango wa ruzuku wa Marekani kwa ajili ya wafanyabiashara wake.

Soma Zaidi:Makamu wa rais wa bunge la Ulaya ashtakiwa kwa rushwa

Macron amesema viongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya watajadili jinsi watakavyo jibu hatua ya rais wa Marekani Joe Biden kuhusu mkakati wake wa kupunguza mfumuko wa bei nchini mwake. Macron amesisitiza kuwa ili kudumisha ushindani wa haki, Ulaya ni lazima irahisishe sheria zake za ruzuku haraka ili ziwe sawa na kile ambacho Marekani inafanya. Umoja wa Ulaya hapo awali ulitahadharisha kwamba ruzuku za Marekani zinaweza kuwa zinakiuka sheria za Shirika la Biashara Ulimwenguni WTO ingawa Rais wa Marekani Joe Biden amekataa kubadili mkondo licha ya kuahidi kufanya marekebisho.

Jumuiya ya Umoja wa Ulaya pia imefikia makubaliano ya kujiunga na mpango wa kimataifa, ambapo takriban nchi za ulimwengu 140 zimetia saini juu ya kuzitoza kampuni kubwa za kimataifa kodi ya chini ya asilimia 15. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameipongeza hatua hiyo amesema makubaliano hayo yanalenga kuzizuia nchi kujiamulia kupunguza kodi ili kuzivutia kampuni za kimataifa bila kufwata sheria.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Nicolas Landemard/Le Pictorium/MAXPPP/dpa/picture alliance

Mbali na hayo mkutano wa viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya uligubikwa na suala la kashfa ya ufisadi. Spika wa bunge la Ulaya Roberta Mestola amesema taasisi hiyo italeta mageuzi kadhaa ili kurejesha imani. Mbunge mwandamizi aliyekuwa makamu wa spika anahusika na madai hayo ya ufisadi na amevuliwa madaraka wakati akifanyiwa uchunguzi. Mbunge huyo wa Ugiriki, Eva Kaili amefunguliwa mashtaka.

Vyanzo: AP/RTRE