Ulaya kujiandaa kwa vita vilevile kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 17.09.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Ulaya kujiandaa kwa vita vilevile kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi

Viongozi barani Ulaya wanazingatia uwezekano wa kuiwekea nchi ya Iran vikwazo vya kiuchumi vilevile kujiandaa kwa vita baada kukataa kusitisha sehemu ya mpango wake wa nuklia.Mazungumzo kati ya Iran na Umoja wa mataifa yameambulia patupu vilevile vikwazo vilivyowekwa havijafanikiwa kusitisha mpango wa kurutubisha madini ya urainum.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Bernard Kouchner

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Bernard Kouchner

Bwana Kouchner anasema kuwa hawatokubali kwa bomu la aina hiyo kutengezwa na sharti jamii ya kimataifa ijiandae kwa vita japo hatua ya kutafuta suluhu iko mstari wa mbele .Hata hivyo hakuelezea matayarisho yenyewe.

Kulingana na Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Bernard Kouchner ,Iran inapaswa kuwekewa vikwazo vipya endapo inaendelea kukataa kusitisha mpango wake wa nuklia.Marekani kwa upande wake inaamini kuwa suluhu ya kidiplomasia na kiuchumi ni mwafaka.

''Juhudi za Iran za kuimarisha teknolojia yake huenda zikasababisha silaha za nuklia kutengezwa jambo linalotishia usalama wa eneo linalojulikana kuwa na usalama duni.Vitendo vya Iran vinahatarisha usalama wa mataifa yote kila mahali ndio mana Marekani inataka kuungwa mkono na mataifa yaliyo wandani wake kote ulimwenguni kuitenga na kuiwekea vikwazo vya kiuchumi.Tutapambana na tatizo hili kabla muda haujakwisha''

Makampuni ya Ufaransa ya mafuta ya Total na Gaz de France wanatolewa wito wa kutochukua kandarasi zozote mpya nchini Iran.

Iran kwa upande wake inakanusha katakata madai hayo ya kutaka kutengeza silaha za nuklia na kushikilia kuwa mpango huo unalenga kutengeza nishati kwa wakazi wake.Rais Mahmoud Ahmedinejad anapendekeza kufanywa kwa mjadala wa umma katika baraza la Umoja wa mataifa linalokutana wiki ijayo ili kuamua aliye sahihi kati yake na kiongozi mwenzake wa Marekani.Marekani ilipuuza pendekezo hilo mwaka jana.

Nchi zilizo wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa Uingereza,Uchina,Urusi ,Marekani na Ujerumani wanapanga kukutana Septemba 21 mjini Washington kujadilia rasimu mpya ya azimio la vikwazo dhidi ya Iran.

Wakati huohuo Shirika la Umoja wa mataifa la kusimamia matumizi ya nuklia IAEA linaanza mkutano hii leo mjini Vienna unaozileta pamoja nchi 144 wanachama.Suala la Iran linatarajiwa kuwa mada kuu.Kiongozi wa Shirika hilo Mohemd El Baradei anashtumiwa na mataifa ya magharibi kwa kuwa na msimamo usiokuwa mkali kwa nchi ya Iran.

Makamu wa rais wa Iran Reza Aghazadeh anahutubia kikao hicho kinachohudhuriwa pia na viongozi wa sekta za nishati wa Marekani na Urusi.

Shutma hizo dhidi ya Bwana Mohamed El Baradei zinakita katika makubaliano kati ya Shirika la IAEA na Iran yanayoeleza kuwa mpango wake wa nuklia ni wa kutengeza nishati pekee shughuli ambayo inaweza kuchunguzwa.

Marekani kwa upande wake inahofia kuwa Iran huenda ikatumia mbinu hii ili kuepuka kuwekewa vikwazo vipya kwa kukataa kusitisha mpango wa kurutubisha madini ya uranium.Mpango huo unatengeza nishati ya nuklia ila unaweza kutumika kama mali ghafi ya kutengeza silaha za nuklia.

Suala nyeti ni namna ya kupata hakikisho kuwa mpango huo unalenga kutengeza nishati pekee.Marekani inashinikiza Iran kuwekewa vikwazo zaidi na Umoja wa mataifa huku Bwana El Baradei akitilia mkazo ukaguzi utakaosababisha mazungumzo kufanyika ili kutafuta suluhu.

Mkutano huo wa wiki moja unafanyika ikiwa ni kumbukumbu ya 50 tangu kuanzishwa kwa shirika hilo.

 • Tarehe 17.09.2007
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB1C
 • Tarehe 17.09.2007
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB1C

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com