1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya kuiwekea Belarus vikwazo vikali zaidi

Lilian Mtono
21 Juni 2021

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa wanachama awa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuiwekea vikwazo vikali zaidi Belarus, wakilenga sekta zitakazokuwa na athari kwenye utawala wa taifa hilo.

https://p.dw.com/p/3vID7
Portugal Lissabon | EU-Außenministertreffen
Picha: Armando Franca/AP Photo/picture alliance

Mawaziri wa mambo ya kigeni waUmoja wa Ulaya wamekubaliana kuiwekea vikwazo vikali zaidi Belarus, wakilenga sekta zitakazokuwa na athari kwenye utawala wa taifa hilo, hii ikiwa ni kulingana na wanadiplomasia.

Mawaziri hao wa Umoja wa Ulaya wanaokutana Luxembourg Jumatatu hii wamekubaliana kuongeza shinikizo dhidi ya rais wa Belarus Alexander Lukashenko kwa kuidhinisha vikwazo vikali zaidi dhidi ya makampuni yanaoyoungwa mkono na serikali, wamesema wanadiplomasia.

Makubaliano hayo yamefikiwa kwenye mkutano mjini Luxembourg kufuatia wiki kadhaa za mazungumzo magumu kuhusiana na sekta gani ya kiuchumi wangeigusa kwa kuiwekea vikwazo. Hatua hiyo kali bado inatakiwa kuidhinishwa rasmi.

Soma Zaidi: Lukashenko kukabiliwa na vikwazo vya EU?

Vikwazo hivyo vinatarajiwa kuvilenga vyanzo vya mapato vinavyounufaisha utawala wa Belarus kama uuzwaji nje wa mbolea, sekta ya tumbaku na mafuta ghafi pamoja na sekta ya kifedha, wanadiplomasia waliliambia shirika la habari la AFP.

Kulingana na wanadiplomasia wa Ulaya, waliozungumza na vyombo mbalimbali vya habari, mawaziri hao wa kigeni wanaokutana Luxembourg pia walijadiliana kuweka vikwazo 80 zaidi kwa watu binafsi na mashirika kuanzia kuzuia mali zao hadi kuzuia hati zao za kusafiria.

Belarus Minsk | Rede Alexander Lukashenko im parlament
Rais wa Belarus Alexander Lukashenko anakabiliwa na shinikizo kubwa dhidi ya madai ya ukiukwaji wa haki za binaadamu nchini humo. Picha: Maxim Guchek/BELTA/AFP via Getty Images

Heiko Maas ataka vizuizi zaidi

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas ametoa mwito wa vikwazo vipana zaidi vya kiuchumi dhidi ya Minsk, akiangazia tukio la ndege ya shirika la ndege la Ryanair kushushwa kwa lazima, ili kumkamata mwandishi wa habari ambaye ni mkosoaji mkubwa wa serikali. Alitoa mwoti huo alipozungumza na gazeti la Ujerumani la Die Welt.

Rais wa Belarus, Lukashenko aliibua ukosoaji mkubwa baada ya kuagiza ndege hiyo iliyokuwa ikitokea Ugiriki kuelekea Luthuania, kubadilisha njia na kulazimika kutua Minsk, kabla ya kumkamata mwandishi huyo wa habari Raman Pratasevich pamoja na rafiki yake wa kike Sofia Sapega, aliyekuwa akisafiri naye.

Soma Zaidi: Viongozi walaani kukamatwa mwanaharakati wa Belarus

Umoja wa Ulaya mara kadhaa ulilifungia shirika la ndege la Belarus kupita kwenye anga la wanachama wake, wakati pia ikizuia mashirika yake kutumia anga la Belarus.

Lukashenko ametawala Belarus tangu 1994. Amekuwa pia akikabiliwa na shinikizo kutoka mataifa ya magharibi, huku akiungwa mkono na rais wa Urusi Vladimir Putin.

Kiongozi wa upinzani anayeishi uhamishoni Sviatlana Tsikhanouskaya anayeendelea kusisitiza kwamba alishinda kwenye uchaguzi mkuu mwaka jana, alifanya mazungumzo na mawaziri hao kabla ya mkutano huo wa kilele Jumatatu hii.

Mashirika: AFPE/DPAE/DW