1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya inapaswa kuchukua njia yake

Daniel Gakuba
29 Mei 2017

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amezitaka nchi za Ulaya kusimamia yenyewe mustakabali wake, akisema wakati wa kuwategemea washirika wa kijadi umekwisha. Hayo yanafuatia mkwamo katika mikutano ya kilele ya NATO na G7.

https://p.dw.com/p/2dj8g
München Bierzeltauftritt von Angela Merkel
Kansela Angela Merkel katika kampeni jimboni BavariaPicha: picture-alliance/dpa/S. Hoppe

Kauli hiyo Kansela Angela Merkel ameitoa wakati wa kampeni ya chama chake cha Christian Democratic Union -CDU jimboni Bavaria jana Jumapili. Bi Merkel ambaye anawania muhula wa nne katika uchaguzi wa Septemba mwaka huu, amesema mkutano wa kilele wa nchi saba zinazoongoza kiviwanda, G7, umekuwa kama kengele ya kumzindua mtu kutoka usingizini.

Viongozi wa G7 walishindwa kukubaliana juu ya mkataba wa kimataifa wa Paris unaolenga kupunguza ongezeko la joto duniani, baada ya Rais  wa Marekani Donald Trump aliyekuwa akishiriki mkutano huo kwa mara ya kwanza, kusema anahitaji muda zaidi kabla ya kufanya maamuzi.

Kansela Merkel alisema ushirikiano wa kijadi katika nchi za Magharibi siyo kitu ambacho nchi za Ulaya zinaweza kuendelea kukitegemea bila mashaka yoyote.

''Wakati ambapo tunaweza kutegemea kikamilifu ushirikiano wa washirika wetu, kwa kiasi fulani umekwisha, kulingana na niliyoyashuhudia mnamo siku chache zilizopita. Sisi watu wa Ulaya tunapaswa kuweka mustakabali wetu mikononi mwetu.'' Amesema Merkel, huku akipendekeza kuendelea kuwepo urafiki na Marekani, Uingereza, na inapowezekana, pia urafiki na Urusi na nchi nyingine.

Italien G7 - Angela Merkel und Donald Trump
Misimamo ya Rais Donald Trump iliwatatiza viongozi wa NATO na G7.Picha: picture-alliance/ZUMAPRESS/C. Minelli

''Lakini tunapaswa kujua kuwa sisi kama watu wa Ulaya inatubidi kupigania mustakabali wetu wenyewe. Hicho ndicho ambacho ningetaka tufanye pamoja''. Amesisitiza Kansela Merkel.

Matokeo ya kukatisha tamaa

Tayari  Merkel alikwishadokeza hali hiyo mara tu baada ya mkutano wa kilele wa G7 uliofanyika nchini Italia, akesema ulikuwa wenye matatizo kupita kiasi, na kwamba matokeo yake hayakuwa ya kuridhisha hata kidogo.

Ripoti nyingi kutoka mkutano huo zilielezea tofauti za wazi baina ya Rais Donald Trump kwa upande mmoja, na vingozi wa nchi sita zilizosalia kwa upande mwingine. Nchi hizo ni Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Canada na Japan. Kwa pamoja nchi saba zilipata muafaka juu ya lugha kuhusu malengo ya kibiashara, lakini ilipokuja kwenye kwenya suala la mkataba wa ulinzi wa mazingira, Trump alijitenga na wenzake. Merkel hali kadha amezungumzia upinzani mkali ulioibuka kuhusu suala la kuongeza msaada kwa ajili ya wakimbizi.

Schulz ataka Trump akabiliwe bila mzaha

Mpinzani mkuu wa Kansela Merkel katika uchaguzi wa Septemba, kiongozi wa chama cha Social Democratic Martin Schulz pia ameingilia kati, akisema kupitia mahojiano na kituo cha utangazaji cha ARD, kwamba jibu muafaka kwa msimamo wa Rais Trump kutaka kufanya kila kitu peke yake, ni nchi za Ulaya kuimarisha zaidi mshikamano wao.

Schulz ameonya dhidi ya kumchukulia Trump kimzaha, akisema anaamini lingekuwa jambo la busara, kama viongozi wengine wangekuwa wameelezea bayana misimamo yao katika mkutano wa NATO, na hususan katika mkutano wa G7, akilinganisha tabia ya Rais Trump kama ile ya viongozi wa kiimla, wanaofurahia kuwaaibisha wengine.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, dpae

Mhariri: Caro Robi