1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yazungumzia kujiuzulu kwa May

24 Mei 2019

Kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Theresa May kunaonekana kuwa huenda kukaifanya hali ya Uingereza kujiondoa kutoka kwenye Umoja wa Ulaya, Brexit, kuwa ngumu zaidi.

https://p.dw.com/p/3J2Gr
Belgien Brexit-Gipfel in Brüssel
Picha: Reuters/Y. Herman

Haya yanajiri huku wengine wakisema kuwa kwa sasa uwezekano wa Uingereza kuondoka katika Umoja huo bila makubaliano ni jambo ambalo hawawezi kuliepuka.

Umoja wa Ulaya umesema kuwa kujiuzulu kwa May hakutabadilisha kwa njia yoyote ile msimamo wake kuhusu yale waliyokubaliana na na Uingereza mwezi Novemba. Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker kupitia msemaji wake Mina Andreeva amesema uamuzi wa kujiuzulu kwa May ni jambo ambalo limemhuzunisha.

"Tumeweka msimamo wetu katika makubaliano ya kujiondoa na katika azimio la kisiasa, Baraza la Umoja wa Ulaya na kifungu cha hamsini limeweka msimamo wake na tuko tayari kabisa kwa yeyote atakayekuwa Waziri Mkuu mpya."

Ujerumani itaendelea kushirikiana vyema na Uingereza

Naye msemaji wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Martina Fietz, amesema Kansela huyo anauheshimu uamuzi wa May akidai kuwa walikuwa na mahusiano mazuri ya kuaminiana katika utenda kazi.

Belgien Brexit-Gipfel in Brüssel | May & Merkel
Theresa May(kushoto) akiwa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kulia)Picha: Reuters/K. Tribouillard

Akiapa kuendelea kufanya kazi na May kama kawaida katika muda wote atakaokuwa afisini Merkel amesema Ujerumani inataka kuendeleza ushirikiano na mahusiano mazuri na serikali ya Uingereza.

Fietz lakini amekataa kutoa maoni alipoulizwa ni vipi kujiuzulu kwa May kutakavyouathiri mchakato wa Brexit akisema inategemea zaidi na jinsi hali ya kisiasa itakavyokuwa Uingereza.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron naye ameusifu uamuzi wa May wa kudhamiria kufanikisha Brexit kama walivyotaka raia wa nchi yake na wakati huo huo akionyesha heshima kwa washirika wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya.

Uhispania pia imetoa kauli kuhusiana na hatua hiyo aliyochukua May ya kuondoka afisini Juni 7 ambapo kupitia msemaji wa serikali Isabel Celaa, imeonya kuwa huenda Uingereza ikaondoka Ulaya bila makubaliano.

Uhusiano wa Urusi na Uingereza ulikuwa mbaya katika uongozi wa May

"Katika hali hii, Brexit bila makubaliano inaonekana ni hali ambayo Uingereza haiezi kuiepuka. Serikali ya Uingereza, bunge la Uingereza ndio wa kulaumiwa kwa nchi yao kuondoka bila makubaliano na athari zake."

Frankreich Präsident Macron trifft britische Premierministerin Theresa May
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu MayPicha: Reuters/P. Wojazer

Urusi nayo kupitia msemaji wa Rais wa Urusi Vladimir Putin, Dmitry Peskov imesema muhula wa May kuongoza umekuwa kipindi kigumu sana kwa mahusiano ya nchi hizo mbili.

Shinikizo kutoka kwa wabunge wa chama cha Kihafidhina cha May ambao walikuwa hawayataki makubaliano yake ya Brexit zilikuwa zimezidi katika miezi michache iliyopita. Mwezi Machi alilazimika kukiri kuwa atajiuzulu iwapo bunge litayakataa makubaliano yake kwa mara ya nne baada ya kuyakataa mara tatu alipoyawasilisha.