1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukunga wa jadi waruhusiwa tena Malawi

16 Machi 2011

Wakati serikali ya Malawi iliporuhusu wakunga wa jadi kutoa huduma, akina mama wajawazito wengi walifurika nyumbani kwa Dorothy Chirwa wa kijiji cha Malombe, wilaya ya Mangochi Kusini mwa mto Malawi.

https://p.dw.com/p/10aQv
Akinamama wa Malawi
Akinamama wa MalawiPicha: DW / Thomas Mandlmeier

Mkunga huyo ni miongoni mwa maelfu ya wakunga wa jadi waliopigwa marufuku na serikali nchini Malawi kutoa huduma ya uzazi mwaka 2007. Wakati huo, Wizara ya Afya ilikuwa imesema kuwa vifo vingi vya akinamama vilitokana na ujuzi mdogo wa wakunga hao.

Wizara hiyo ilisema wakunga wa jadi hawakuwa na uwezo wa kugudua kwa haraka matatizo ya uzazi yanayohitaji huduma za dharura, na pia kushindwa kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka mama kwenda kwa motto.

Rais wa chama cha madaktari wa magonjwa ya wanawake, Dk. Frank Taulo, amesema kipindi ambacho wakunga hao walipokuwa kwenye marufuku hiyo, matatizo ya uzazi, kama kupasuka kwa mji wa uzazi au kibofu cha mkojo, yaliyokuwa yanatishia maisha ya akina mama wajawazito wakati wa kujifungua, yalipungua

Mwanamke wa Malawi akipika
Mwanamke wa Malawi akipikaPicha: DW / Thomas Mandlmeier

Mwaka 2007, idadi ya vifo vya akina mama nchini Malawi ilikuwa 807 kwa wanawake 100, 000 wanaojifungua. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa kwenye mkutano wa kupitia upya mikakati ya mpango wa malengo ya milenia mwaka jana, idadi hiyo ilikuwa imeshuka hadi kufikia 510.

Mkurugenzi mtendaji wa mhirika la manesi na wakunga nchini Malawi, Dorothy Ngoma, amesema licha ya mafanikio hayo, mfumo hafifu wa afya uliwafanya wanawake wengi kuendelea kufuata huduma ya uzazi kwa wakunga wa jadi, pamoja na marufuku iliyowekwa.

Anasema wakunga wa jadi, walijificha kwa kuhofu kukamatwa na kutozwa faini, kutokana na kujificha kwao, takwimu za akina mama waliopoteza maisha mikononi mwa wakunga hao wajadi, hazijulikani.

Dk. Taulo amesema wanawake wajawazito hawapati huduma ya afya ya kutosha na chama chake mara kadhaa kimetoa mapendekezo ya kuongeza vituo vya afya, kutoa mafunzo kwa watu wengi na kuwarudisha manesi na maafisa wa afya waliostaafu ili kufidia mapungufu yaliyopo katika kutoa huduma ya uzazi badala ya kuwahusisha watu wasio na ujuzi.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni kutoka wizara ya afya, nafasi mbili kati ya tatu katika sekta ya afya nchini Malawi ziko wazi.

Aliporudi kutoa wenye mkutano wa kuangalia upya mikakati ya mpango wa malengo ya milenia mwaka jana, Rais wa Malawi, Bingu wa Mutharika aliwashangaza wengi alipobadili maamuzi yake kuhusu wakunga wa jadi.

Rais Mutharika alisema wakunga wa jadi wasikatazwe kutoa huduma kwa akina mama wajawazito, badala yake wapewe mafunzo kuhusu njia bora za kutumia wakati wanapotoa huduma hiyo.

Mara baada ya tamko hilo la rais, wanawake wajawazito wakafurika nyumbani kwa Chirwa, kilometa 70 kutoka hosptali ya wilaya ya Mangochi inayotoa huduma za uzazi.

Hata hivyo, Chirwa anakubali kuwa huduma anayotoa kwa jamii yeye pamoja na wakunga wengine wa jadi, sio kamilifu.

Anasema wakati mwingine yanatokea matatizo ambayo hawezi kuyashughulikia kutokana na ujuzi mdogo, lakini hawezi kukataa kutoa huduma hiyo kwa akina mama wanaohitaji msaaa wake.

Chama cha Madaktari wa mangojwa ya akina mama, hawakufurahishwa na uamuzi huo wa Rais Mutharika, na kuuliza pakitokea matatizo ya uzazi, wakunga hao watayashughulikia vipi wakati hawana vifaa?

Mwandishi: Rose Athumani/IPS
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman