1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine,Scottland na Polisi wa Sheria magazetini

8 Septemba 2014

Hali mashariki ya Ukraine,kura ya maoni ya Scottland na mjadala kuhusu "Polisi ya sharia" Wuppertal na kuwashawishi wapita njia ni miongoni mwa mada magazetini nchini Ujerumani

https://p.dw.com/p/1D8dx
Miripuko yaripotiwa Donetsk licha ya makubaliano ya kuweka chini silahaPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Grits

Tuanzie lakini Ukraine ambako licha ya makubaliano ya amani kutiwa saini ijumaa iliyopita,pande zinazohasimiana zinalaumiana kuyaendeya kinyume.Viongozi wa magharibi wanatahadharisha.Gazeti la "Donaukurier" linaandika:"Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinemeir hajakosea alipozungumzia wasi wasi kama makubaliano ya kuweka chini silaha yataheshimiwa.Mkataba huo unaangaliwa kama kipindi kifupi cha kuvuta pumzi-fursa ndogo ya kutafakari.Ndio maana nchi za magharibi zinabidi kufanya kila liwezekanalo ili kutoipoteza fursa hiyo.Kutunisha misuli na kufanya luteka za kijeshi pamoja na kuipatia silaha serikali ya mjini Kiev sio dawa,kinachohitajika ni juhudi kubwa zaidi za kidiplomasia pamoja na Kiev na Moscow.

Mzozo wa Ukraine umewafanya wajerumani wabadilishe msimamo wao kuelekea jumuia ya kujihami ya NATO.Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaandika:"Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliosimamiwa na kituo cha kwanza cha matangazo ya Televisheni nchini Ujerumani-ARD,kwasasa ni asili mia nane tu ya wajerumani wanaohisi jumuia ya NATO haina maana-miaka mitano iliyopita,idadi yao ilifikia asili mia 12.Chanzo cha hali hii ni kiu cha kujizidishia madaraka rais wa Urusi Vladimir Putin.Umoja wa fakhari wa Usovieti umevunjika sawa na zilivyotawanyika nchi za mkataba wa Warsaw.Ukuta wa Berlin umeporomoka mwaka 1989.Matarajio ya walimwengu hivi sasa ni kushuhudia ukuta mpya ukivunjika Gorbatchov mwengine akichipuka na kumng'owa madarakani Putin.

Hatima ya Umoja wa Ulaya baada ya Kura ya maoni ya Scottland

Kura ya maoni itakayoamua kama Scottland iendelee au la kuwa sehemu ya Uingereza inawakosesha usingizi sio tu viongozi wa serikali mjini London bali pia wale wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels.Gazeti la "Volksstimmen" la mjini Magdeburg linaandika:"Saa mashuhuri ya Big Ben ya mjini London inastahiki kuanzia sasa kuonya usiku na mchana:Uingereza,tangu miaka 300 iliyopita haijawahi kujikuta hatarini kama sasa.Wakaazi wa Scottland wanapigania kujitenga-nchi hiyo ya kifalme ya Uingereza inatishia kudhoofika-kitakuwa kishindo kikubwa kwa malkia,waziri mkuu,wakaazi wa Uingereza na hata kwa Umoja wa Ulaya.Kwasababu licha ya hofu zote kuelekea sarafu ya Euro,Uingereza ni mmojawapo ya mihimili ya Umoja wa ulaya.Brussels itakabiliana vipi na Uingereza iliyogawika?Kamishna wa masuala ya mtengano hajatajwa katika orodha ya makamishna itakayotangazwa wiki hii na kiongozi wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya Jean Claude Juncker.Isingekuwa vibaya lakini tukizingatia vitisho kama hivyo kutoka Kataloni nchini Hispania na kwengineko.

Flagge Scottland
Bendera ya ScottlandPicha: AP Graphics

Wafuasi wa Itikadi kali Wuppertal

Tumalizie yaliyoandikwa magazetini kwa mjadala uliozuka humu nchini baada ya kundi la wafuasi wa itikadi kali kuteremka majiani mjini Wuppertal wakivalia vikoti vilivyoandikwa "Polisi ya sharia".Gazeti la "Nordbayerische Kurier" linaandika:"Kwa mkumbo mmoja nchi imekurupuka:"Polisi ya sheria mjini Wuppertal" imewagutua wananchi.Hatimae watu wanatambua hatari inayotokana na wafuasi wa itikadi kali wasioijali serikali.Cha kutia moyo ni ile hali kwamba vyama vyote vya kisiasa vimesimama kidete kupambana na hatari hiyo-hata kama kuna wanaotaka kuitumia hali hiyo kujipendekeza.Watambue tu wanapovutana juu ya nani kashindwa kufanya nini katika juhudi za kupambana na wafuasi wa itikadi kali,wanawapa nguvu wafuasi wa siasa kali tu za mrengo wa kulia.

Scharia-Polizei in Wuppertal
Polisi ya Sharia mjini Wuppertal-Bwana mmoja wa Cologne anafuatilizia ripoti kuhusu tukio hiloPicha: picture-alliance/dpa/O. Berg

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu