1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yaitaka NATO kuyakataa madai ya Urusi

Josephat Charo
3 Desemba 2021

Ukraine imesema inakataa juhudi zozote kufuta mipango yake ya kujunga na jumuiya ya kujihami ya NATO pamoja na hakikisho lolote linalotafutwa na Urusi kwa lengo la kupunguza msuguano na hali ya wasiwasi mpakani.

https://p.dw.com/p/43obF
Strategischer Dialog zwischen USA und Ukraine
Picha: Leah Millis/AP/Reuters/dpa/picture alliance

Msuguano kati ya urusi na Ukraine umeendelea kushika kasi leo huku waziri Kuleba akisema Ukraine kukubali kufutilia mbali mipango yake ya kujiunga na NATO si suala la kufikirika wala chaguo kwa serikali na amelipinga wazo kwamba wanatakiwa kuihakikishia Urusi kitu chochote.

Akizungumza na shirika la habari la AFP pembezoni mwa mkutano wa shirika la ushirikiano wa ulinzi barani Ulaya, OSCE, mjini Stockholm nchini Sweden, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba, amesisitiza kuwa ni Urusi ndiyo inayotakiwa kuhakikisha haitaendelea na uchokozi wake dhidi ya nchi yoyote na ameitaka NATO iyakatae madai ya Urusi.

"Tunakaribisha mazungumzo katika ngazi zote. Nimefanya mkutano muhimu na wa maana na waziri Blinken hapa Sweden. Tumekubaliana kuratibu kwa pamoja kabla mazungumzo kati ya rais Biden na Putin na pia kitakachotokea baadaye. Tuna imani na washirika wetu, na wao wana imani na sisi. Sidhani chochote kitaamuliwa kati yao kinyume na masilahi ya Ukraine."

Rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin wanatarajiwa kufanya mazunguzo katika siku zijazo kuhusu hali ya wasiwasi nchini Ukraine, takriban miaka saba tangu Urusi ilipolitwaa eneo la Crimea na waasi wanaoegemea upande wa Urusi kudhibiti sehemu ya mashariki ya Ukraine.

Lavrov ahimiza subira

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov amemtaka mwenzake wa Marekani Anthony Blinken kutoa hakikisho kwamba NATO haitasogea karibu na mipaka ya Urusi. Lavrov amesisitiza juu ya kuandaa orodha jumla ya mambo inayotaka ihakikishiwe ili usalama wa kila upande, na ule wa washirika wote katika mchakato mzima wa Umoja wa Ulaya.

Antony Blinken und Sergei Lawrow
Mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani, Anthony Blinken, kushoto, na mwenzake wa Urusi, Sergei LavrovPicha: Russian Ministry of Foreign Affairs/TASS/imago images

Lavrov amesema hataki kubashiri kuhusu ukweli kwamba nchi za Magharibi zinaweza kutia munda na kukataa kutafakari na kuyazingatia mapendo ya Urusi yatakayowasilishwa na amependekeza pawepo subra kuona hatua itakayochukuliwa na viongozi wa Ulaya.

"Jambo la muhimu ni kuona jinsi gani jumuiya ya nchi za magharibi itakavyoyachukulia kwa uzito mapendekezo yetu, ni kwa umbali wanamaanisha na ikiwa wataka kweli kupunguza msuguano na kutuliza hali ya wasiwasi na machafuko."

Wakati hayo yakiarifiwa waziri wa ulinzi wa Ukraine Oleksii Reznikov, akinukuu taarifa za kijasusi, ameliambia bunge leo kwamba Urusi imewapeleka wanajeshi zaidi ya 94,000 karibu na mpaka wa Ukraien na huenda inajiandaa kufanya harakati kubwa ya kijeshi mwishoni mwa mwezi Junauri mwakani.

(afp,reuters)