1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yafanya duru ya pili uchaguzi wa Rais

21 Aprili 2019

Raia nchini Ukraine wanamiminika vituoni leo Jumapili kwa duru ya pili ya uchaguzi usio wa kawaida, ambapo mchekeshaji kwenye vipindi vya televisheni anatazamiwa kushinda.

https://p.dw.com/p/3HAKO
Ukraine Präsidentschaftswahl 2019 | Debatte - Poroschenko vs. Selenskyj
Picha: Getty Images/AFP/S. Chuzavkov

Uchunguzi wa maoni ulikuwa unaonesha kuwa Volodymyr Zelensky mwenye umri wa miaka 41 angelimshinda rais wa sasa, Petro Poroshenko, huku kukiwa na hasira za wapigakura dhidi ya umasikini na ufisadi.

Vituo vya kura vilifunguliwa saa 11 alfajiri na kutazamiwa kufungwa saa 11 jioni, na matokeo ya awali kujulikana masaa kadhaa baadaye.

Ushindi wa Zelensky ulitazamiwa kufunguwa ukurasa mpya wa historia ya nchi hiyo ambayo imekumbwa na mapinduzi ya umma mara mbili ndani ya miongo miwili na inakabiliwa na vita vya waasi wanaotaka kujitenga tangu mwaka 2014.

Ukraine inategemea misaada ya kimataifa na nishati kutoka Urusi, na rais ajaye wa taifa hilo atapaswa kukabiliana na Rais Vladimir Putin wa Urusi na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Tambo zahanikiza uchaguzi wa leo

Ukraine Präsidentschaftswahl 2019 | Debatte - Poroschenko vs. Selenskyj
Picha: Getty Images/B. Hoffman

Poroshenko mwenye umri wa miaka 53 alijenga hoja kwamba Zelensky ni mpya kwenye siasa na hafai kuwa amiri jeshi mkuu wakati wa vita.

Lakini muigizaji huyo wa vichekesho aliwekeza kwenye hasira za umma dhidi ya rushwa, umasikini na vita ambavyo vimeshauwa takribani watu 13,000.

"Kuna matumaini kwamba mtu huyu wa kawaida anaweza kutufahamu zaidi na kuuporomoa mfumo tulionao nchini mwetu," alisema Yuliya Lykhota, mwenye umri wa miaka 29 na anayemuunga mkono Zelensky. "Ni jambo muhimu sana kuinuwa hamasa ya watu wetu."

Wengine wanashuku endapo Zelensky, anayefahamika zaidi kwa kucheza nafasi ya rais katika kipindi cha televisheni kiitwacho "Mtumishi wa Watu", ataweza kuyabeba maslahi mapana ya taifa.

"Siamini kama atakaa muda mrefu baada ya kuchaguliwa," amesema Serhiy Fedorets, mwenye umri wa miaka 62. "Hana uungwaji mkono bungeni. Watamla mzima mzima."

Zelensky kuwa rais ajaye?

Ukraine Schauspieler Volodymyr Zelensky
Picha: picture-alliance/Pacific Press/A. Gusev

Uchunguzi wa maoni ulioendeshwa na taasisi ya Rating wiki hii ulionesha kwamba Zelensky atashinda kwa asilimia 73 ya kura dhidi ya 27 za Poroshenko.

Poroshenko aliingia madarakani baada ya mapinduzi ya umma yaliyokuwa na vurugu mwaka 2014 kuuondowa utawala uliokuwa ukielemea Kremlin, na kuchochea hatua ya Urusi kuuchukuwa mkoa wa Crimea.

Hata hivyo, wengi miongoni mwa raia milioni 45 wa Ukraine wanahisi kuwa ahadi za mapinduzi hayo yaliyoungwa mkono na madola ya Magharibi hazijatimizwa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Rashid Chilumba