1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Ukraine: Urusi inaishikilia Belarus kama “mateka wa nyuklia“

26 Machi 2023

Ukraine imesema hayo baada ya rais wa Urusi Vladimir Putin kutangaza kwamba atahifadhi silaha za kimkakati za nyuklia nchini Belarus.

https://p.dw.com/p/4PG4B
Russland | Alexander Lukaschenko und Wladimir Putin
Picha: Mikhail Klimentyev/Sputnik/Kremlin Pool Photo via AP/picture alliance

Katibu wa Baraza la Usalama wa Kitaifa na Ulinzi wa Ukraine Oleksiy Danilov ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba "Urusi imeichukulia Belarus kama "mateka wa nyuklia". Ameongeza kuwa hatua hiyo inaelekea kuvuruga utulivu  wa Belarus.

Rais wa kiimla wa Belarus Alexander Lukashenko ambaye amekuwepo madarakani kwa takriban miaka 30 ni mshirika wa karibu wa Rais Putin wa Urusi.

Mnamo Jumamosi, Putin alisema yeye na Lukashenko "wamekubaliana” kwamba Urusi itahifadhi silaha za nyuklia nchini Belarus, "bila ya kukiuka makubaliano ya kimataifa kuhusu kutoeneza" zana za nyuklia.

Vikosi vya Urusi vyabadili mwelekeo wake Bakhmut

Mnamo Jumapili, Mykhaylo Podolyak mshauri wa rais wa Ukraine, aliishutumu Urusi kwa "kukiuka mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia".

"(Putin) amekiri kwamba anaogopa kushindwa, kwa hivyo anachokifanya ni kutisha watu," Podolyak alisema hayo pia kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Mnamo mwezi Februari 2022, Minsk iliiruhusu Kremlin kuanzisha uvamizi nchini Ukraine huku vikosi vyake vikitokea upande wa Belarus.

Hofu imekuwa ikiongezeka kuwa huenda Belarus ikajiunga na Urusi kuisaidia kwenye uvamizi huo, lakini Lukashenko amesema atafanya hivyo "ikiwa tu atashambuliwa".

Lukashenko: Tunaiunga mkono China kuhusu Ukraine

Kulingana na Danilov, tangazo la Putin linazidisha kiwango cha mtizamo mbaya watu wanao dhidi ya Urusi na Putin katika jamii ya Belarus.

Rais wa China Xi Jinping 8kushoto) na Rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa China Xi Jinping 8kushoto) na Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: SERGEI KARPUKHIN/AFP

Putin: Urusi na China haziundi muungano wa kijeshi

Rais Putin amesema nchi yake na China haziundi muungano wa kijeshi na kwamba hazifichi chochote kuhusiana na ushirikiano wao wa kijeshi.

Amesema hayo siku ya Jumapili alipohojiwa kwenye kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali ya nchi yake.

"Hatuundi muungano wowote wa kijeshi na China,” kituo cha Interfax kilimnukuu Putin akisema. "Ndiyo tuna ushirikiano katika nyanja za kiufundi wa kijeshi. Hilo hatufichi. "Kila kitu kiko wazi, hakuna siri.”

Putin pia alisema mataifa ya Magharibi yanajaribu kuunda miungano ya kimataifa, huku akiishutumu Marekani na Jumuiya ya Kujihami ya NATO kwa kuanza kuunda muungano mpya unaofanana na uliojumuisha Ujerumani, Italia, na Japan wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Mapema wiki hii, Putin na rais wa China Xi Jinping walipofanya mkutano wa kilele,, walisifu kile walichokitaja kuwa ‘enzi mpya ya uhusiano' na kuahidi kuimarisha ushirikiano wao. Hayo yanajiri mnamo wakati Urusi inajitahidi kupiga hatua mbele kwenye kile inachokiitza ‘operesheni spesheli ya kijeshi' nchini Ukraine

Vyanzo: AFPE, RTRE