1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine kulipanga upya jeshi lake Mashariki mwa nchi hiyo

Mjahida10 Septemba 2014

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko amesema anawapanga upya wanajeshi wake Mashariki mwa nchi hiyo ili kuboresha ulinzi wake dhidi ya watu wanaotaka kujitenga Mashariki mwa nchi hiyo wanaoiunga mkono Urusi.

https://p.dw.com/p/1D9ml
Rais Petro Poroshenko wa Ukraine
Rais Petro Poroshenko wa UkrainePicha: Reuters/Vasily Fedosenko

Rais Poroshenko ameliambia baraza lake la mawaziri mjini Kiev kwamba hatua hiyo ni ya kujilinda pekee. Matamshi ya rais huyo yanakuja wakati kukiwepo makubaliano ya usitishwaji wa mapigano yanayoyumba. "Hii sio kwa sababu ya mashambulizi ni njia tu ya kulilinda eneo letu," Alisema rais Poroshenko na kunukuliwa na vyombo vya habari nchini Ukraine.

Hata hivyo mapigano kati ya vikosi vya serikali na watu wanaotaka kujitenga Mashariki mwa nchi hiyo yamepungua kufuatia pande zote mbili hasimu kutia saini makubaliano ya kusitisha mapigano ijumaa iliopita katika mji mkuu wa Belarus Minsk baada ya miezi takriban mitano ya mapigano.

Aidha rais Poroshenko amesema hali imebadilika tangu makubaliano hayo yatiwe saini lakini akasema pia utekelezaji wake umekuwa wa mashaka kufuatia wale aliowaita magaidi kujaribu mara kwa mara kuvichokoza vikosi vya Ukraine.

Rais Petro Poroshenko na Waziri wake Mkuu Arseny Yatsenyuk
Rais Petro Poroshenko na Waziri wake Mkuu Arseny YatsenyukPicha: Reuters/Andrew Kravchenko

Poroshenko amesisitiza kwa mara nyengine tena kwamba makubaliano ya minsk hayamaanishi Ukraine iliachie eneo lake la Mshariki kutekwa na watu wanaotaka kujitenga anaowaita magaidi.

OSCE yapanga kutuma ndege zisizokuwa na rubani Ukraine

Kwa upande mwengine shirika la usalama la ushirikiano barani Ulaya kupitia mwenyekiti wake Didier Burkhalter limesema litapelekea ndege zisizokuwa na rubani nchini Ukraine kufuatilia usitishwaji wa mapigano. Burkhalter ambaye pia ni rais wa Uswisi amesema ndege hizo zitapelekwa hivi karibu lakini hakutaja tarehe kamili ya kufanya hivyo.

Huku hayo yakiarifiwa mabalozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana hii leo mjini Brussels kujadili namna ya kuiwekea Urusi Vikwazo vipya kufuatia vitendo vyake nchini Ukraine.

Vikwazo hivyo vitalenga kuizuwia Urusi kuingia katika masoko ya fedha na mauzo ya nje katika Umoja wa Ulaya, marufuku mpya ya kusafiri na kuzuwiya kwa mali za viongozi wa juu wa Urusi na hata waasi wanaotaka kujitenga.

Baadhi ya waasi wanaotaka kujitenga Mashariki mwa Ukraine
Baadhi ya waasi wanaotaka kujitenga Mashariki mwa UkrainePicha: Reuters

Wengi wa wanachama wa Umoja wa Ulaya wanataka kuendelea na vikwazo hivyo huku wengine wakihofia kuukwaza uchumi wa mataifa yao na hata kuyumbisha makubaliano ya kusitisha mapigano iwapo wataendelea kuiwekea Urusi vikwazo. Urusi kwa upande wake imeapa kujibu vikwazo hivyo.

Kwengineko shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limesema lina ushahidi wa kutosha kwamba pande zote mbili zimetekeleza uhalifu wa kivita katika mzozo wa Ukraine.

Kulingana na katibu mkuu wa shirika hilo Salil Shetty, Urusi pia imechangia pakubwa katika mzozo wa Ukraine lakini Urusi kwa upande wake imeendelea kukanusha madai hayo.

Mwandishi Amina Abubakar

Mahriri: Iddi Ssesanga